The House of Favourite Newspapers

Mwalimu Asakwa Kwa Kumbaka Mwanafunzi Ngorongoro

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Olenasha.

NAIBU Waziri wa Elimu,  Sayansi na Teknolojia, William Olenasha, ameagiza kukamatwa kwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Loliondo,  Erick Kalaliche,  kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wake wa kidato cha tatu (jina limehifadhiwa) ambaye kwa sasa amehamia mkoa wa Lindi baada ya kutenda kosa hilo.

 

Akizungumza katika kikao cha dharura kilichofanyika  makao makuu ya Halmashauri ya Ngorongoro,  Olenasha amesema jambo hilo linasikitisha na kuidhalilisha sekta ya elimu na lazima hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe mara moja.

 

Amesema wizara yake haiwezi kuvumilia walimu ambao wanafundisha watoto ambao pia ni kama wazazi,  wanaofumbia macho vitendo  vichafu ambavyo vinarudisha nyuma sekta ya elimu na juhudi za serikali kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

 

Ofisa Elimu wilaya ya Ngorongoro, Emanuel Sukuma,  amekiri mwalimu huyo kutenda kosa la kumbaka mwanafunzi huyo ambapo kitendo hicho kilifanyika mwezi wa tatu na kujulikana mwezi wa sita ambapo hakuna hatua zozote za kinidhamu zilizochukuliwa.

 

Amesema kuwa mwalimu Erick alimchukua mwanafunzi huyo ambaye alikuwa anasoma kidato cha tatu katika shule hiyo na kumpeleka nyumba ya kulala wageni na kumbaka.

 

Tarehe 9 Julai, mwaka huu,  Olenasha alifanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo na kuhoji kuhusu taarifa za mwalimu huyo ambapo mwalimu mkuu, Neema Mchao,  alikosa majibu sahihi lakini baadaye kukiri kwamba mwalimu huyo alihama shuleni hapo na alikuwa ametenda kosa hilo.

 

Mchao alikiri kufuatilia jambo hilo lakini alipohojiwa kwa nini hakuchukua hatua za kinidhamu,  alisema yeye aliachia mamlaka husika kwa sababu hata yeye jambo hilo lilimsikitisha.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngorongoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya, Rashidi Mfaume Taka,  amesema utaratibu unafanyika  wa kurudishwa Ngorongoro kwa mwalimu huyo kutoka mkoa aliohamishiwa kuwa kitendo alichokifanya ni udhalilishaji katika wilaya hiyo.

 

Kufuatia kikao hicho, Mkuu wa Polisi wilayani Ngorongoro amemtaka Mchao, na Ofisa Elimu kufika kituoni  kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

Comments are closed.