visa

MWALIMU AUAWA KWA KISU NA MWANAUME

MWALIMU wa Shule ya Msingi Liwiti jijini Dar, aliyetambulika kwa jina la Selani Hamisi ameuawa kwa kuchomwa kisu na mwanaume anayedaiwa kuwa ni mtu wake wa karibu. 

 

Chanzo kinaeleza kuwa, tukio hilo lilitokea Mei 6, mwaka huu ambapo mwalimu huyo alikuwa akitokea shuleni kwake akiwa na wanaye wawili. “Huyo mwanaume alimvizia njiani, alipofika karibu yake alimkimbilia na kumchoma kisu shingoni kilichoutoa uhai wa mwalimu huyo,” kilisema chanzo.

 

MDOGO WA MAREHEMU AFUNGUKA

Akizungumza na Risasi Jumamosi mdogo wa marehemu aitwaye Baraka Hamisi Kondo alisema kuwa, alipigiwa simu na kaka yake kuelezwa habari ya tukio lililompata dada yao wakati akitoka shuleni kwake. “Nilienda eneo la tukio kwa bahati mbaya nilimkuta dada ameshafariki dunia na walimu wenzake walikuwa wanatusubiri sisi ndugu ili twende kuripoti polisi.

 

“Bahati nzuri watoto aliokuwa nao dada yangu walimuona aliyemchoma kisu na wakamtambua,” alisema mdogo huyo wa marehemu na kutaja jina la mtuhumiwa ambalo Risasi Jumamosi inalihifadhi kwa sasa kutokana na maadili. Inaelezwa kuwa, mara baada ya mtuhumiwa huyo kufanya unyama huo alipanda kwenye bodaboda ambayo inadaiwa aliikodi kisha kutokomea kusikojulikana.

 

Kisa cha mauaji hayo hakijawekwa wazi na mamlaka za usalama wa raia, lakini habari za chini ya kapeti zinadai kuwa, mwanaume anayetuhumiwa kwa mauaji alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu lakini kutokana na kushindana tabia alimuacha. Kitendo hicho cha kumwagwa wakati akiwa bado anampenda marehemu, ndicho kinasimuliwa kuwa kilimtia chuki mtuhumiwa hadi kufikia hatua ya kufanya mauaji ya kinyama.

MJUMBE ASIMULIA TUKIO

Mjumbe wa Shina Namba 6, Merry Mkiwa ambaye anaishi karibu na Shule ya Msingi Liwiti jijini Dar alisema alipata taarifa kupitia mjukuu wake ambaye ni mwanafunzi wa shule hiyo.

 

“Mjukuu wangu alikuja mbio nyumbani na kuniambia kuwa amemuona mwalimu wao amechomwa na kisu, ikabidi niende mpaka pale nikamkuta amelala chini, nikafanya mawasiliano na ndugu, jeshi la polisi na wote walifika mapema. “Polisi walipomaliza kufanya vipimo vyao eneo la tukio wakauchukua mwili wa marehemu hadi kituoni na kisha ukapelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuhifadhiwa,” alisema mjumbe huyo.

 

KAMANDA ATHIBITISHA

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Zuberi Chembela alipotafutwa kwa njia ya simu na Risasi Jumamosi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Taarifa hizi zimenifikia, kwa sasa tunafanya taratibu za kujua kuhusu aliyehusika na tukio hilo, upelelezi wetu bado unaendelea,” alisema kamanda huyo.

Tambwe Afunguka kurogwa na Donald Ngoma
Toa comment