Mwalimu mbaroni ubakaji wa mwanafunzi ofisini

JESHI la polisi Mkoa wa Mara limemkamata mwalimu wa Shule ya Msingi ya Bwai A, Lazaro Mmanga, kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) wa miaka 14, darasa la saba.

Taarifa zinasema mwalimu huyo aligutukiwa na marafiki wa mwanafunzi anayedaiwa kufanya naye tendo hilo baya.

“Ni kwamba wanafunzi wale baada ya kuona mwenzao akiingia chumbani kwa kupitia dirishani, walikwenda kuchungulia na kuona kila kitu,” alisema mtoa habari kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini.

Alisema, wanafunzi hao walikwenda kuripoti tukio hilo kwa viongozi wa serikali ya kijiji ambao walifika haraka na kukuta mwalimu akiwa bado yupo ndani na denti huo.

Akithibitisha habari hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Juma Ndaki, alikiri kutokea kwa tukio hilo Septemba 4 mwaka huu.

“Wanafunzi hao walisema walimshuhudia mwalimu huyo akimpitisha mwanafunzi mwenzao dirishani na baada ya muda kutoka nje na kisha kumfungia ndani ya ofisi hiyo ambapo baada ya wanafunzi hao kuona tukio hilo walikwenda moja kwa moja kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za kijiji eneo hilo,” alisema kamanda.

Kamanda Ndaki alisema, uongozi wa kijiji ulilitaarifu jeshi la polisi ambapo kwa haraka walifika shuleni hapo na kufanikiwa kumkamata mwalimu huyo na kumfikisha katika Kituo cha Polisi cha Mgango.

Kamanda Ndaki alisema kuwa, kabla ya kufanikiwa kumtia mbaroni mwalimu,  askari hao walikuta umati mkubwa uliokuwa umezingira ofisi hiyo ya mwalimu mkuu wakizuia askari wasimkamate mwalimu huyo aliyekuwa ndani kwani walikuwa wamekusudia kumuua.

“Askari polisi hao walipambana na wananchi waliowazuia kumtia mbaroni mtuhumiwa wakitaka kumuua, walilirushia mawe gari la polisi lenye namba za usajili PT 1441 Toyota Land Cruiser na kuliharibu,” alisema kamanda.

Akifafanua zaidi Ndaki alisema katika hatua za kuokoa gari hilo jitihada zilifanyika baada ya askari polisi kurusha risasi hewani kutawanya watu lakini kutokana na wingi wao, walijaribu kuchoma moto gari hilo lakini baadhi ya raia wema na askari polisi walifanikiwa kuuzima kabla ya kuleta madhara.

Wakati huohuo jeshi la polisi limewakamata watu wawili kwa kosa la kupatikana na injini za boti 10, mali zinazodhaniwa za wizi baada ya kufanyika misako maeneo mbalimbali katika Wilaya za Musoma, Bunda, Butiama na Serengeti tangu Agosti 29 hadi Septemba 5 mwaka huu mkoani hapa.

Kamanda  Ndaki aliwataja waliokamatwa  na mali hizo kuwa ni  Walagai Masoya maarufu kama Nyajirali aliyekamatwa Septemba tatu mwaka huu katika maeneo ya Bwai,  na Mwinyi Eunyo aliyekamatwa Septemba 3 mwaka huu akiwa na injini sita za boti.

Ndaki alisema kuwa watu hao wanaendelea kushikiliwa na uchunguzi unaendelea kufanyika ili hatua za kisheria zichukuliwe
Toa comment