The House of Favourite Newspapers

Mwalimu Mkuu Mbaroni Manyara!

0

MANYARA: Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, imemtia mbaroni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Orkitikiti, Oscar Waluye. Shule hiyo ipo katika Kijiji cha Engong’ongare wilayani Kiteto.

 

Waluye yupo korokoroni kwa tuhuma ya kufanya udanganyifu wa mitihani ya darasa la saba, iliyofanyika wiki iliyopita hapa nchini.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, mtuhumiwa huyo akiwa ni mwalimu mkuu wa shule hiyo, aliwalazimisha wanafunzi wawili wa darasa la sita, kufanya mitihani ya darasa la saba, badala ya watahiniwa ambao uwezo wao darasani unaelezwa kuwa ni mdogo.

 

Mwalimu huyo pia anatuhumiwa kukaririsha mwanafunzi mmoja na kuwaingiza kwenye chumba cha mtihani wanafunzi wawili wa darasa la sita, pamoja na mwanafunzi aliyehitimu shule mwaka jana, kufanya mtihani huo.

 

Kamanda wa Takukuru wilayani Kiteto, Mkungu alisema baada ya kupata taarifa hizo, walifika shuleni hapo na kuwakuta wanafunzi hao wakiwa wameshafanya mitihani ya masomo ya Kiswahili na Hisabati, kinyume na sheria kwa kuwatumia wanafunzi wasiostahili kufanya mitihani hiyo.

 

Alidai kuwa, wanafunzi hao mamluki, walikuwa wanafanya mitihani hiyo kwa niaba ya wenzao wa darasa la saba ambao wanadaiwa kuwa na uwezo mdogo, huku aliyekaririshwa akitumia jina la mwanafunzi mtoro shuleni hapo.

 

Alisema kuwa, uchunguzi unaendelea na utakapokamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mwalimu huyo, ambapo alitoa wito kwa walimu kufanya kazi kwa uadilifu, kulea watoto katika njia ipasayo, ikiwa ni pamoja na kusoma kwa bidii badala ya kufanya udanganyifu katika mitihani.

 

Alisema kuwa, Takukuru hawatomuonea haya mtu yeyote atakayekiuka sheria za nchi, kwani kwa kufanya hivyo, ni kukiuka sheria na taratibu na pia linatengenezwa kundi la wasiojua kusoma na kuandika ingawa wataonekana walifaulu.

Stori: Mohamed Hamad, Ijumaa

Leave A Reply