The House of Favourite Newspapers

Mwalimu Nyerere Anavyoishi Ndani ya JPM

WAKATI leo Watanzania wakiadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 tangu rais wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere afariki dunia, baadhi ya malengo na maono yake kwa Tanzania yamefufuliwa na kuanza kutekelezwa chini ya uongozi wa Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli, Ijumaa Wikienda linachambua.

 

Nyerere ambaye alikuwa ni Baba wa Taifa, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza na kuzikwa Butiama mkoani Mara.

 

Licha ya kutokuwepo kwa miaka 20 sasa, baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wanamuona anaishi ndani ya Rais John Magufuli kutokana na tabia pamoja na kasi ya utekelezaji wa baadhi ya mambo aliyoyaanzisha Mwalimu Nyerere na kukwama kwa sababu mbalimbali.

 

Mojawapo ya maono hayo aliyoyaasisi Mwalimu Nyerere na sasa yanatekelezwa na Rais Magufuli ni pamoja na ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Rufiji, Serikali kuhamia Dodoma, Muundo mpya wa CCM, Nidhamu serikalini, utetezi wa wanyonge na hulka ya ukali.

 

MIRADI

Katika moja ya jambo lililoasisiwa na Mwalimu Nyerere na kutekelezwa na Rais Magufuli ni ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa maji la Mto Rufiji, lililopewa jina la Julius Nyerere.

 

Hoja hiyo inaungwa mkono na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi ambaye alibainisha kuwa mpango huo uliasisiwa na Baba wa Taifa lakini ukakwama kutokana na sababu mbalimbali lakini sasa ujenzi wake umeanza na unatarajiwa kuzalisha Megawati 2,115.

 

KUHAMIA DODOMA

Mpango wa Serikali kuu kuhamia makao makuu Dodoma ni moja ya jambo lililotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano licha ya mchakato huo kuanza mwaka 1973 baada ya kuasisiwa na Mwalimu Nyerere, lakini mpango huo ulikwama kutokana na mdororo wa vita vya Iddi Amin mwaka 1978.

 

Kwa mujibu wa aliyekuwa waziri wa serikali ya awamu ya kwanza, Balozi Job Lusinde alinukuliwa akibainisha wazi kuwa kuanzia mwaka 1973 wizara zilikuwa zimeanza kuhamia Dodoma lakini mchakato huo ukakwamishwa na vita hiyo iliyosababisha mdororo wa kiuchumi.

 

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Profesa Kabudi wakati akizungumza katika kongamano la kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere lililofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam ambaye aliongeza kuwa mbali ya vita hiyo ya Uganda pia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ndiyo chanzo cha kukwama kwake.

 

MUUNDO MPYA WA CCM

Katika moja ya mambo ambayo yalianza kutekelezwa na Rais John Magufuli alipoingia madarakani Novemba 5, mwaka 2015 ni kupunguza utitiri wa vyeo ndani ya Chama Cha Mapinduzi ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya chama hicho.

 

Mmoja wa wanasiasa wakongwe walionukuliwa kupongeza muundo huo ni Dk Chrisant Mzindakaya ambaye alisema muundo huo umedhihirisha Mwalimu Nyerere anaishi ndani ya Rais Magufuli kwa kuwa na muundo huo wa idadi ndogo ya watendaji makini unaosaidia kulinda siri za chama, kubana matumizi na kuwajibika ipasavyo kuisimamia Serikali.

 

Disemba 2016, Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kwa kupitia vikao vya Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC), idadi ya wajumbe wa NEC ilipunguzwa kutoka wajumbe 388 hadi wajumbe 158, huku wajumbe wa CC wakipunguzwa kutoka 34 hadi 24.

 

TABIA ZA UKALI

Ukali ni mojawapo ya sifa ya Rais Magufuli hasa kutokana na hulka yake ya kutumbua vigogo wanaoonesha kushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Hulka hiyo inalandana na ile ya Mwalimu Nyerere ambaye pia wakati mwingine alikosana na waliokwenda kinyume cha Katiba na kufikia hata hatua ya kuwaweka kizuizini.

 

Tabia hizo za ukali kwa namna moja au nyingine pia zimekuwa zikichangia kurudisha nidhamu serikalini ambapo hata Rais Magufuli mwenyewe mara kadhaa amekuwa akinukuliwa akisema kuwa anainyoosha Serikali hivyo Watanzania wamvumilie.

 

KUTETEA MASKINI NA WANYONGE

‘Mimi ni rais wa maskini’, hili ni mojawapo ya neno ambalo limekuwa likitajwa na Rais Magufuli kila mara hususani awapo katika ziara mbalimbali mikoani kuzungumza na wananchi jambo linalodhihirisha kuwa ni Mwalimu Nyerere anaishi ndani yake.

 

Mwalimu Nyerere alitetea maskini, wanyonge ambapo moja ya mambo aliyoamini, kuyatenda na kuyasimamia kwa nguvu zote ni kuwasaidia Watanzania maskini na wanyonge wanaoonewa.

 

Kuifanya Ikulu mahali patakatifu

Aidha, Ijumaa Wikienda limebaini kuwa katika moja ya hotuba za Baba wa Taifa, aliyoitoa Mei Mosi 1995 jijini Mbeya alikaririwa akisema kuwa ‘Ikulu ni mahali patakatifu’ kwa maana kuwa si pango la wanyang’anyi au sehemu ya kwenda kufanya biashara.

 

Vivyo hivyo Rais Magufuli alidhibitisha hilo baada ya kusafisha Ikulu kwa kufuta idara mbalimbali na kurejesha hadhi ya Ikulu kama ilivyokuwa zamani.

 

Itakumbukwa kuwa punde baada ya kuingia Ikulu Novemba 5, mwaka 2015 Rais Magufuli alifuta kitengo cha mapokezi ya wageni kwenye lango kuu la Ikulu na kuagiza watendaji wa serikali katika ngazi zote kutatua kero za wananchi mahala walipo ili kuwapunguzia usumbufu.

STORI: GABRIEL MUSHI, DAR

Comments are closed.