The House of Favourite Newspapers

Mwambusi Aanza na Sare Yanga

0

BAO la David Bryson dakika ya 28, jana liliishtua Yanga wakati ikikabiliana na KMC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Bryson alifunga bao hilo kwa shuti kali akiwa nje ya 18 akitumia mguu wa kushoto na kumshinda mlinda mlango wa Yanga, Farouk Shikhalo.Kuingia kwa bao hilo, kukawafanya Yanga kujipanga upya kurudisha mashambulizi kwa wapinzani wao, lakini hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika, hawakufanikiwa kupata bao na kuiacha KMC ikienda mapumziko kwa uongozi wa bao 1-0.

Kipindi hicho cha kwanza, ilishuhudiwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Abdoul Razack mapema tu dakika ya kwanza akitafuta nafasi ya kufunga, lakini akakwama.Yanga waliokuwa wakifanya mashambulizi mengi upande wa KMC, ilishuhudiwa ikipata kona ya kwanza dakika ya 13, ambayo haikuwa na madhara.

Hadi KMC wanapata bao hilo, Yanga ilipata faulo nne karibu na lango la KMC, lakini mpigaji, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, alishindwa kuzitumia vema ambapo kipindi cha kwanza chote, Mrundi huyo alipiga jumla ya faulo sita zilizokuwa hazina faida.

 

Maelekezo waliyopewa nyota wa Yanga wakati wa mapumziko na Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi, yalizaa matunda mapema tu kipindi cha pili ambapo dakika ya 46, Yacouba Songne aliukwamisha mpira wavuni kwa kichwa.

Fiston ambaye alionekana hana madhara kwenye mchezo wa jana, alitolewa dakika ya 62 na nafasi yake kuchukuliwa na Deus Kaseke.

 

Hadi mwisho wa mchezo huo, Yanga 1-1 KMC na kuifanya Yanga kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 51 kutokana na kucheza mechi 24, inafuatiwa na Azam yenye pointi 47 kwa mechi 25 na Simba pointi 44, mechi 20.Huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza wa Mwambusi tangu akabidhiwe kikosi hicho baada ya kuondolewa kwa Cedric Kaze, Machi 7, mwaka huu.

Leave A Reply