Mwambusi Ataja Mambo Manne Yanga

KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi, ameanza kuonesha moto ndani ya timu hiyo baada ya kuwapa wachezaji wake mambo manne anayotaka kuyaona.

 

Mwambusi anakaimu nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mrundi, Cedric Kaze aliyetimuliwa Machi 7, mwaka huu kufuatia mwenendo wa matokeo ya kusuasua licha ya Yanga kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi kuu Bara ikiwa na pointi 50, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 46.

 

Yanga kwa sasa imekuwa ikijiandaa na mechi za ligi na Kombe la FA ikiwa chini ya Mwambusi ambaye amekuwa akiwasisitizia nyota wake mambo manne wanapokuwa mazoezini.

 

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kambi ya timu hiyo iliyopo Avic Town, Kigamboni, Dar ambazo Spoti Xtra imezipata, zinasema kuwa kocha huyo amekuwa mkali kuhakikisha kikosi chake kinarudisha hali ya kujiamini na kupata ushindi.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Mwambusi amekuwa akisisitiza suala la nidhamu kwa wachezaji kwa kuwa ndiyo nguzo kubwa ambayo inaweza kuwabeba kufanya vizuri katika michezo yao.

 

“Timu inaendelea na mazoezi kwa muda mrefu licha ya kwamba baadhi ya nyota hapo awali kukosekana kutokana na kuwa na majukumu kwenye timu zao za taifa.

 

“Kocha amekuwa akiwasisitiza wachezaji kwanza kuwa na nidhamu kwa kuwa ndiyo msingi mkubwa wa mafanikio, lakini pia wakubali kujitolea kwa sababu wameajiriwa na Yanga kuipa mafanikio na mafanikio hayo hayawezi kutokea kama watashindwa kuwa hivyo.

 

“Pia amewataka wachezaji kuelewa kwamba hakuna atakayekuwa na namba ya kudumu kwenye timu, hivyo kila mmoja anatakiwa kujituma na jambo la mwisho kutambua kama bado wanapigania ubingwa na hawapaswi kushuka katika nafasi waliyopo sasa,” alisema mtoa taarifa huyo.

STORI: IBRAHIM MUSSA, Dar es SalaamTecno


Toa comment