The House of Favourite Newspapers

Mwamnnyeto: Yanga Itawavua Simba Ubingwa Msimu Huu

0

JOTO la msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara linazidi kushika kasi, wakati huu ambapo zimesalia siku tatu pekee kabla ya filimbi ya kuanza rasmi kwa michezo ya ligi hiyo kupulizwa mnamo Septemba 27, mwaka huu kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini.

 

Msimu mpya unaanza katika wakati ambao tayari klabu zimekamilisha maboresho ya vikosi vyao kupitia dirisha la usajili wa nyota wapya, ambalo lilifungwa Agosti 31, mwaka huu.

 

Miongoni mwa klabu ambazo zimefanya usajili mkubwa katika dirisha lililopita la usajili ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga, ambao wanajinasibu kuwa msimu huu wana jambo lao.

 

Kuelekea msimu wa 2021/22, Yanga imekamilisha usajili wa nyota wapya 11 kutoka mataifa mbalimbali ambao ni; Heritier Makambo na Fiston Mayele, Yusuph Athuman, makipa Djigui Diara na Erick Johora, mabeki Djuma Shabani na Bryson Raphael pamoja na viungo, Khalid Aucho, Yannick Bangala Litombo, Dickson Ambundo na Jesus Moloko.

 

Championi Ijumaa, limepiga stori na nahodha wa Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto ambaye amefunguka mambo mengi kuhusiana na kikosi chao kwa msimu wa 2021/22 kama ifuatavyo;

 

MALENGO YENU MSIMU UJAO NI YAPI?

“Malengo yetu makubwa msimu ujao ni kuhakikisha tunashinda angalau kombe moja kubwa katika michuano ambayo tunakwenda kushiriki, hususani kombe la Ligi Kuu Bara.

 

UNAUZUNGUMZIAJE USAJILI ULIOFANYWA NA YANGA?

“Naupongeza uongozi kwa kuwa umefanya usajili mzuri, na ambao umeangalia upungufu wa kikosi chetu kwa msimu uliopita na kuurekebisha, kuna wachezaji ambao walikuwepo msimu uliopita ambao wamebaki lakini pia wapo nyota wapya ambao wamekuja kutuongezea nguvu kwa ajili ya msimu unaoanza.

 

Siri ya mafanikio yako kusalia ndani ya kikosi cha Yanga ni ipi?

“Binafsi nadhani vitu vikubwa ambavyo vimenisaidia kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu ni ile hali ya kuwa makini kusikiliza maelekezo ya mwalimu, lakini pia kujituma sana katika mazoezi na kuhakikisha ninakuwa sawa kisaikolojia.

 

Usajili wa mchezaji gani umekuvutia zaidi?

“Kwangu naweza kusema usajili wote ambao umefanyika ndani ya Yanga ni usajili bora, kwa kuwa kila mtu katika nafasi yake amekuwa akifanya kazi nzuri kwa ajili ya kuisaidia timu.

 

“Tuna matumaini makubwa kupitia uzoefu wa nyota wapya waliojiunga nasi, na ule wa wachezaji tuliokuwa na timu kwa msimu uliopita tutakuwa na nafasi ya kutimiza malengo yetu.

 

Unapata ugumu gani kuongoza mastaa walio kwenye timu yenu?

“Ugumu upo kwa kiasi fulani kwa kuwa unapokuwa nahodha lazima uongoze kwa mifano na haupaswi kufanya makosa ya kizembe.

 

“Hiyo ndiyo changamoto ambayo kwa kiasi fulani imekuwa ikinisumbua lakini sio ukubwa wa majina, kwa kuwa kila mtu anapokuwa uwanjani anakuwa kiongozi wa mwenzake kwani hata mimi binafsi naweza kufanya makosa na wenzangu wana wajibu wa kunirekebisha.

 

Unajisikiaje kupata nafasi ya kucheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza?

“Ni jambo la furaha sana kwangu kuwa sehemu ya wachezaji ambao wamepata nafasi ya kushiriki mashindano haya makubwa, hasa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

 

“Kufikia hatua hii ni utimilifu wa malengo na ndoto ambazo nimewahi kuwa nazo, licha ya kwamba kwa bahati mbaya hatukufanikiwa kufika mbali kama ambavyo tulitarajia.

 

Kuachwa kwa baadhi ya nyota waliokuwepo msimu uliopita kumepelekewa na nini?

“Mi naamini wachezaji wote walioachwa ni wachezaji wazuri lakini zipo changamoto nyingi ambazo zinaweza kutokea hasa unapojiunga na timu mpya.

 

“Kuna wakati mchezaji unaweza kushindwa kufiti kwenye mfumo wa mwalimu na kupelekea mchezaji kukosa nafasi, lakini pia kuna wakati inaweza kuwa ni upepo tu.

 

NI KWELI TIMU YENU INAKOSA MUUNGANIKO?

“Kikosi chetu kimefanya usajili wa baadhi ya nyota wapya ambao ni wazi wanahitaji muda wa kuzoea mazingira na kujifunza utamaduni wa soka letu, hivyo bado kwa kiasi fulani tunahitaji muda wa kuzidi kuzoeana na kuwa na muunganiko utakaoweza kutoa matokeo chanya.

 

KUNA PENGO LOLOTE KUTOKANA NA KUONDOKA KWA ALIYEKUWA NAHODHA WENU LAMINE MORO?

“Kama mchezaji mwenzangu ninamisi kwa kuwa nimewahi kucheza naye, lakini kuhusu kazi naweza kusema hakuna pengo lolote, kwa kuwa mimi naweza kucheza na nyota yeyote, cha msingi ni kuhakikisha kuwa tunaelewana na kufanya kazi vizuri.

 

UNAUZUNGUMZIAJE MCHEZO WA NGAO YA JAMII DHIDI YA SIMBA?

“Tunajua utakuwa mchezo mgumu kama ilivyo kawaida, lakini tumejiandaa vizuri na uwepo wa baadhi ya nyota ambao walikosekana katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United, umetuimarisha zaidi katika ari yetu ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo wa Jumamosi.”

Joel Thomas, Dar es Salaam

Leave A Reply