Mwamuzi wa mchezo wa leo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga, Jonesia Rukyaa.
Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
MWAMUZI wa mchezo wa leo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga, Jonesia Rukyaa, amepokea vitisho kutoka kwa mashabiki wa timu hizo na tangu juzi alikuwa mafichoni jijini Dar es Salaam.
Jonesia anayetokea mkoani Kagera, amekuwa akipokea vitisho hivyo tangu alipotangazwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchezesha mechi hiyo.
Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa Jonesia, mwamuzi huyo amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa mashabiki wa timu zote mbili kila upande wakimtaka kutoipendelea timu nyingine.
“Yaani ni tabu tupu kwani mashabiki wa Yanga wanamtisha asiipendelee Simba na wale wa Simba nao wanamtisha asipendelee Yanga, wanamchanganya tu.
“Lakini mwenyewe anasema yupo imara na yupo hapa Dar es Salaam katika eneo ambalo hakuna anayeruhusiwa kulijua ili kuogopa mambo tofauti kutoka kwa mashabiki hao wanaomtisha,” alisema rafiki huyo.
Hii ni mara ya pili kwa Jonesia kuchezesha mechi ya Simba na Yanga baada ya kufanya hivyo Desemba 13, 2014 katika mchezo wa Nani Mtani Jembe ambapo Simba ilishinda mabao 2-0.
Katika mchezo wa leo, Jonesia atasaidiwa na Josephat Bulali (Tanga), Samwel Mpenzu (Arusha) huku mwamuzi wa akiba akiwa Elly Sasii (Dar) na Kamisaa ni Khalid Bitebo wa Mwanza.