The House of Favourite Newspapers

MWANAKWAYA AMUUA MWANAKWAYA MWENZAKE

KABLA tukio la kusikitisha la Naomi Marijani, mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, kudaiwa kuuawa na mumewe kisha mwili wake kuchomwa moto halijapoa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limetoa tuhuma mpya kwamba mwanakwaya mmoja, mkazi wilayani Maswa anadaiwa kumuua kinyama mwanakwaya mwenzake; Risasi Mchanganyiko linakusimulia tukio zima.

Mtuhumiwa aliyetiwa mbaroni kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP Deusdedit Nsimeki ni Emmanuel Julius, akibanwa kwa mauaji ya Julieth Josephat ambaye mbali na kuwa mwanakwaya mwenzake katika Kanisa Katoliki Nyalikungu, Maswa mjini, lakini pia alikuwa ni mkewe.

“Tunamshikilia huyu mwanaume (Emmanuel) kwa tuhuma za mauaji ya mkewe, kwa kweli ni tukio baya ambalo tunalichunguza kwa umakini na baada ya hapo tutamfikisha mtuhumiwa mahakamani,” alisema kamanda huyo.

MAMA WA MAREHEMU ASIMULIA

Akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu, mama wa marehemu aitwaye Rosemary Jeremiah, alisema tukio hilo lilijiri Julai 12, mwaka huu.

“Siku hiyo watoto wa marehemu walikuja kwangu baada ya kuambiwa na baba yao waje kunisalimia.

“Ilipofika majira ya saa saba mchana, marehemu mwanangu alinipigia simu akaniambia niwaruhusu watoto wake hao wawili (majina yao yanafichwa) warudi nyumbani wakachukue fedha kwa ajili ya kununulia mboga.

“Mimi nikamwambia kuliko waende na kurudi watasumbuka, nikawapa hela wakanunue mboga na kuzipeleka,” alisema mama wa marehemu.

WAFIKISHA MBOGA, WAONDOLEWA

Bila kujua kitakachotokea siku hiyo, watoto hao walidaiwa kufikisha ile mboga kisha baba yao kuwataka kurudi tena kwa bibi yao ambako si mbali na hapo walipokuwa wanaishi wanandoa hao.

“Nilipowaona wamerudi tena kwangu nikawauliza kulikoni? Wakaniambia baba yao kawaambia waje kwangu kwa sababu yeye na mama yao (marehemu) watatoka na kwamba funguo watazificha sehemu ambayo aliwaonesha.

“Mimi nikaendelea kufanya shughuli zangu, ilipofika saa moja jioni niliwaambia wale watoto waende nyumbani kwao,” alisema mama wa marehemu Julieth.

WATOTO WAKUTA DAMU NDANI

Kwa mujibu wa chanzo kutoka eneo la tukio kilidai kuwa, baada ya watoto wale kufika nyumbani kwao walikwenda mahali walipokuwa wameelekezwa kuukuta ufungua, lakini haukuwepo.

Baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kuwasubiri wazazi wao warejee kutoka matembezini kama walivyokuwa wameambiwa bila mafanikio waliamua kwenda kumuomba mama mwenye nyumba awaangalizie ufunguo wa akiba ili waweze kuingia ndani ambapo walipewa.

Kwa mshangao watoto hao walipofungua mlango na kuingia ndani walikutana na dimbwi la damu lililowafanya wapigwe na butwaa.

Inaelezwa kuwa, watoto hao walipowasha taa na kuangalia kwa umakini walimuona mama yao akiwa kitandani amelowa damu, wasijue kuwa ameshaaga dunia.

Kutokana na hali hiyo walitoka nje kuwaita majirani ambao walikuja na kushuhudia mauaji ya kutisha ambayo yaliwafanya wenye mioyo miepesi kuangua

kilio huku wakificha nyuso zao wasione kilichokuwa kimefanyika nyumbani humo kwa watu ambao wamedaiwa kuwa wanakwaya wenye mahudhurio mazuri kanisani.

MWILI WAKUTWA NA MAJERAHA YA KUTISHA

Kwa mujibu wa shuhuda mmoja akiwemo mama mzazi wa marehemu aliyefika eneo la tukio kujionea mauaji hayo ya kutisha inadaiwa kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umepigwa mara tatu kichwani na kitu kizito kilichotajwa na mashuhuda hao kuwa ni nyundo.

Mbali na kichwa hicho kuonekana kupigwa, mwili wa marehemu Julieth ulikutwa pia na majeraha yanayodaiwa kuwa ni ya kisu sehemu mbalimbali za mwili.

“Shingoni kulikuwa na majeraha makubwa mawili, mwilini yalikuwepo kama manne hivi na tumbo lilikuwa limetobolewa na utumbo ulikuwa nje.

“Kusema kweli mwanangu ameuawa kinyama sana sijui alikosa kitu gani kikubwa cha kutendewa ukatili huo,” alisema mama wa marehemu kwa uchungu alipokuwa akizungumza na mwanadishi wetu.

SABABU YA MAUAJI I HII

Vyanzo mbalimbali vililiambia Risasi Mchanganyiko kuwa sababu ya mauaji hayo ya Julieth ni ileile iliyozoeleka; “Ni wivu wa kimapenzi.”

Kibaya zaidi mmoja wa watu wa karibu na marehemu alisema aliwahi kuambiwa na Julieth kuwa mumewe alikuwa akimtuhumu kutoka nje ya ndoa, jambo ambalo si kweli ambapo imedaiwa kuwa huenda sababu hiyo ilichochea kutokea kwa mauaji hao kama vyombo vya sheria vitathibitisha kuwa muuaji ni Emmanuel.

Mama wa marehemu Julieth alikiri kusikia tuhuma hizo kutoka kwa mkwewe na

kuonesha masikitiko yake kwa nini mume huyo wa mwanaye aliyefunga ndoa miaka miwili iliyopita kama ni kweli amehusika na mauaji asitafute suluhu nyingine tofauti na hii ya mauaji ambayo haijamsaidia kutatua tatizo.

MWANAKWAYA ASIMULIA

Mmoja wa wanakwaya wa Kanisa Katoliki la Nyalikungu, Maswa mjini ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema tukio hilo limewasikitisha sana.

“Sisi kama watu tunaohudumu kanisani tulitakiwa kuwa mbali na matukio kama haya ya kishetani.

“Imetuuma kwa sababu Julieth alikuwa mwanakwaya mwenzetu na hata huyo mumewe.

“Mi’ nadhani sina la kusema zaidi ya kuzidi kujiombea mwenyewe na kumuombea marehemu Julieth apumzike kwa amani.

“Maana kama ni migogoro ya ndoa Julieth na mumewe walikuwa na nafasi ya kuwaona wazee wa kanisa au mapadri na kusuluhishwa kuliko hiki kilichotokea,” alisema mwanakwaya huyo.

KUTOKA KWA MHARIRI

Dawati la Risasi Mchanganyiko linawaomba wananchi wote hasa wanandoa kuacha kujichukulia sheria mkononi badala yake kuishi kwa upendo na kusameheana na pale hayo yanaposhindikana ni vyema kupelekana kwenye vyombo vya sheria.

Pia tunavishauri vyombo vya usalama na idara ya mahakama kutoa ripoti ya adhabu wanazopewa watuhumiwa wa mauaji ya wapenzi wao ili kuweka mzania wa habari za mauaji na adhabu za watuhumiwa; lengo ni kuzidi kuifahamisha jamii kuwa mauaji siyo suluhisho la matatizo ya ndoa, bali ni chanzo cha matatizo mapya.

Comments are closed.