The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Afariki Kwa Kutafunwa Na Nguruwe

 

MWANAMKE mmoja nchini Urusi ameauawa na nguruwe aliokuwa anawafuga baada ya kuanguka kwenye banda la wanyama hao.

 

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Urusi, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 56 alikuwa akiwalisha nguruwe ndipo ghafla akaanguka na nguruwe hao wakamtafuna.

 

Inasadikiwa kuwa chanzo cha kuanguka kwake ilikuwa ni kuzirai ama kupatwa na kifafa.   Tukio hilo limeripotiwa kwenye wilaya ya Malopurginsky jimboni Udmurtia, lililopo katikati ya Urusi.

 

Vyombo vya habari vya Urusi vimearifu kuwa mume wa marehemu alikuwa amelala wakati mkewe alipokuwa akiwahudumia nguruwe hao. Bwana huyo inasemekana alikuwa mgonjwa.

 

Baada ya kuamka alianza kumtafuta mkewe na kukuta mwili wake ndani ya banda la nguruwe.  Inataarifiwa kuwa alifariki baada ya kupoteza damu nyingi. Tayari upelelezi wa polisi juu ya tukio hilo umeshafunguliwa.

 

Oktoba mwaka 2012 tukio kama hilo liliripoptiwa nchini Marekani katika jimbo la Oregon ambapo Bwana Terry Vance Garner, aliyekuwa na miaka 69 wakati huo alienda kuwalisha nguruwe wake lakini hakurejea.

 

Baadaye, familia yake ilikuta mabaki ya mwili wake kwenye banda la nguruwe huku sehemu kubwa ya mwili huo ikiwa imeshaliwa na wanyama hao.

 

Mamlaka za eneo hilo ziliripoti kuwa mmoja wa nguruwe hao hapo awali alishawahi kumng’ata marehemu lakini aliweza kujinasua.

 

Kaka wa bwana huyo, Michael, alidai kuwa nguruwe hao walishawahi kujaribu kumtafuna na yeye ambapo Garner aliahidi kuliua dume kubwa ambalo ndilo lilikuwa tishio zaidi.   Hata hivyo, baadaye alibadili mawazo na kuendelea kuwafuga mpaka pale walipomuua.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.