The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Ajidunga Sindano ya Juisi ya Matunda, Alazwa Mahututi

 

MWANAMKE mmoja nchini China almanusura afariki dunia, baada ya kujidunga yeye mwenyewe sindano iliyosheheni mchanganyiko wa matunda yaliyotengenezwa kwa jitihada za kuwa na afya.

 

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 51, kufuatia kitendo chake hicho, alisababisha madhara kwenye ini, figo, moyo na uharibifu wa mapafu na akawekwa katika uangalizi maalumu kwa muda wa siku tano.

 

Katika sindano aliyojidunga, kulikuwa na mchaganyiko wa matunda tofauti yapatayo ishirini ambayo alijidunga kwenye mishipa ya damu.  Hii ni kwa mujibu wa mfanyakazi mmoja aliyeko katika hospitali yenye ushirika na Chuo Kikuu cha Xiangnan kilichoko mjini Hunan alipozungumza na shirika la utangazaji la Uingereza (BBC).

 

Watumiaji wa mitandao nchini China wanadai kwamba tukio la mwanamke huyo limeibua hisia na uhitaji wa ufahamu wa huduma ya kwanza kwa jamii.

 

 

Inaarifiwa kuwa baada ya kujidunga mchanganyiko huo wa matunda, mwanamke huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, akaanza kujihisi ngozi yake inauma na kugeuka kuwa nyekundu, na joto likawa likiongezeka mwilini wake.

 

Baada ya hali hiyo, alipokwenda hospitalini ikamlazimu kulazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi mnamo tarehe 22 mwezi uliopita, kabla ya kuhamishiwa katika hospitali kuu na baadaye kuruhusiwa. Tukio hilo limezua mjadala na kugeuka kuwa gumzo nchini China katika mitandao ya kijamii ikiwemo mtandao wa kijamii wa Weibo.

 

Zaidi ya watu elfu kumi na moja wa mtandao huo walitumia msemo huu #OldWomanPutsJuiceIntoVeins. Mtu mmoja alinukuliwa akisema inaonekana kwamba ”ujuzi wa matibabu wa umma bado ni mdogo sana.”

Comments are closed.