Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu – 27

“Hapa huyo Edgar kuna ndugu yake wa damu?” alihoji.

“Ndiyo ni mimi tumezaliwa na baba mmoja, mama mmoja,” nilijibu harakaharaka.

“Sawa. Wewe una kazi kubwa sana. Utatakiwa leo hii usiku tuende makaburini kuna kafara za kutoa kule. Lakini jioni, saa kumi na nusu tutakwenda porini kuchuma baadhi ya majani. Unatakiwa uchume wewe ambaye ndugu yako ana matatizo. Leo itabidi mlale hapahapa kisha kesho, tutakwenda mjini kumuibua, sawa?”

“Sawa kabisa, itawezekana kweli?” nikahoji.

“Muulizeni huyu bwana Makang’ako. Aliwahi kuniona nikifanya kazi hiyo. Japokuwa kutakuwa na sharti moja ambalo mtalitekeleza kabla ya zoezi kufanyika.”

Moyo ukapiga paa na kujiuliza ni sharti gani hilo?

SONGA NAYO…

Tulilala pale kwa mganga na usiku tulifanya shughuli zote ambazo alihitaji tufanye. Tulikwenda makaburimi akamchinja njiwa kisha tukaenda kwenye baadhi ya miti iliyo kando ya makaburi na nikaamriwa kuchuma majani yake mawili mawili nikiwa mtupu.

Baadaye niliambiwa nivae nguo kisha tukaanza safari ya kurudi nyumbani kwa mganga. Tulikuwa wawili tu mimi Jerome na mganga wale wenzetu, kaka Ipacho na bwana Makang’ako walikwenda kulala kwenye nyumba ya kulala wageni iliyopo karibu na kwa mganga.

Hawakuhusika kabisa na kafara na ulozi uliokuwa nikifanyiwa. Tulipofika kwa mganga mambo yalikuwa mazito zaidi kwa sababu nilitakiwa nilale kitanda kimoja na nyoka. Sikujua kama yule nyoka alitolewa meno au la! Nilishituka sana baada ya kuambiwa kuwa lazima nilale na nyoka.

“Huyu ni nyoka anayewakilisha majini. Ni mpole wala huna haja ya kuwa na hofu,” aliniambia yule mganga huku moyoni nikiwaza kwamba huenda lile ndilo sharti alilosema mganga huyo kwamba atanipa sharti.

“Kwani hakuna njia nyingine ya kufanya mpaka nilale kitanda kimoja na huyu nyoka?” nilihoji. Mara hata kabla ya mganga yule kujibu, nyoka alisimamisha kichwa chake na shingo ikafura, nikajua kuwa yule nyoka ni kobra.Nilitetemeka kwa woga.

“Usiogope, huyu siyo nyoka kama unavyomuona, ni jini atakayekusaidia sana kumuokoa kaka yako.”

“Lakini mbona amefutua shingo yake?”

“Sasa wewe unashangazwa na kufutua shingo? Hiyo ni kwa sababu ya shaka na hofu yako. Vua shati lala hapo kando yake,” aliamuru yule mganga.

Wakati nakikaribia kitanda yule nyoka alijinyoosha, alikuwa mrefu maana kile kitanda ni cha futi sita na nyoka alikuwa anakaribia mwisho wa kitanda.

“Mbona anajinyoosha?” Nilimuuliza mganga.

“Hayo hayakuhusu kwani ungemkuta amejipindapinda ndiyo ungefurahia?”

Niligoma kulala kwenye kitanda kile chenye nyoka.

“Huu uganga utakushinda kijana.”

“Ngoja niwapigie wenzangu.”

“Uwapigie uwaaambie nini?”

“Niwaambie kuhusu sharti hili.”

“Haisaidii kwa sababu anayetakiwa kulala na nyoka ni wewe na siyo ndugu zako uliokuja nao.”

Wakati mganga anasema hayo nilimpigia simu kaka Ipacho ilikuwa ikiita tu. Nilisubiri apokee ikawa haipokelewi. Nilirudia kupiga hali ikawa ileile. Nilianza kuchanganyikiwa na kujiuliza kulikoni?

Je, kitaendelea nini? Fuatilia Jumanne ijayo.


Loading...

Toa comment