Mwanamke alivyomfanya zezeta kaka yangu – 28

ILIPOISHIA

Wakati mganga anasema hayo nilimpigia simu kaka Ipacho, ilikuwa ikiita tu. Nilisubiri apokee akawa hapokei. Nilirudia kupiga hali ikawa ileile. Nilianza kuchanganyikiwa na kujiuliza kulikoni?

Je, nini kitaendelea?

SONGA NAYO:

Wakati natafakari nini cha kufanya, simu yangu iliita na nilipoiangalia nikaona jina ‘Kaka Ipacho’, moyo wangu ukatulia kudunda.

‘Haloo,” alisema kaka Ipacho.

“Ni mimi Jerome.”

“Ndiyo, nimeona ‘misikolu’ yako nikashtuka, au ulikuwa unatuambia umemaliza kazi na mganga wako?”

“Hapana. Kuna masharti mazito sana, naomba mje tujadili huku mkiona kile kilicho mbele yangu.”

“Ni nini?”

“Njooni bwana, usiku huu kutaja majina mengine ni tabu,” nilisema huku nikimuangalia yule nyoka aliyekuwa akigaagaa kitandani.

Wakati nikizungumza na kaka Ipacho, nilidhani yule mganga alikuwa nyuma yangu, kumbe alikuwa ametoka. Nilishtuka sana kuona nipo peke yangu kwenye kile chumba ambacho kina nyoka.

Nilirudi kinyumenyume hadi nje. Nikawa naangalia ndani na nikaona yule nyoka anashuka kitandani. Nilikimbia mpaka kwenye nyumba ya yule mganga.

“Mzee, mzeee!”

“Vipi tena?” Akasema.

“Yule nyoka ameshuka kitandani,” nilisema huku nikitetemeka kwani nilijua kuwa anaweza akawa ananifuata. Pamoja na mwanga wa taa iliyowashwa pale nje ya nyumba ya mganga, ilinibidi kuwasha tochi yangu ya simu ili kuongeza mwanga, kwani nilijua kuwa yule nyoka ananitaka mimi. Nilikuwa namulika mlango wa kile chumba nilichokuwemo lakini sikuona akitoka.

Yule mganga licha ya kumuambia hivyo akawa hatoki. Niliingiwa na woga huku moyoni nikijiuliza anafanya nini? Au anataka kunitoa kafara? Hata hivyo, maswali yote hayo hayakuwa na jibu.

Wakati natafakari nini cha kufanya nilisikia mlio wa gari, nikajua kwamba hao watakuwa ni kaka Ipacho na bwana Makang’ako. Nilizidi kutetemeka baada ya kuona kitu kikija upande wangu.

“Mzee nakufaaa,” nilipiga yowe.

“Unakufa na nini?” akauliza mganga.

“Nyokaaa, yule nyoka ananijia,” nikajibu huku upepo mkali ukivuma.

“Acha uongo, hawezi kutoka yule,” akasema.

Nilizidi kutumbulia jicho kile kitu kilichokuwa kikinisogelea, kitu kirefu cheusi kama nyoka niliyemuacha ndani ya chumba,

“Baba tafadhali tokaaa,” nikapiga kelele.

Wakati nasema hayo, kaka Ipacho na mzee Makang’ako wakawa wameshafika na wakatoka kwenye gari.

“Vipi?” Waliniuliza baada ya kuona natetemeka.

“Nyoka,” nikawajibu huku nikinyoosha kidole kuelekeza palipo na kile kitu kinachonisogelea.

Mzee Makang’ako alikisogelea kile kitu na akaanza kucheka huku akikishika.

“Huu ni mfuko wa plastiki. Kuna aliyeuchana na kuwa mrefu. Woga gani bwana Jerome huo. Unakuwa kama siyo mwanaume?”

Alikuja mpaka karibu yangu na nikathibitisha kuwa ni mfuko wa plastiki; nilijiona mjinga.

Mzee mganga alitoka chumbani akaanza kusema:

“Huyu ndugu yenu ilitakiwa alale na jini aliye katika umbo la nyoka, ameogopa…

Je, kitaendelea nini? Fuatilia Jumanne ijayo.


Loading...

Toa comment