The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu – 29

0

ILIPOISHIA

Mzee Makang’ako alikisogelea kile kitu na akaanza kucheka huku akikishika.

“Huu ni mfuko wa plastiki. Kuna aliyeuchana na kuwa mrefu. Woga gani huo bwana Jerome. Unakuwa kama siyo mwanaume?”

Alikuja mpaka karibu yangu na nikathibitisha kuwa ni mfuko wa plastiki; nilijiona mjinga.

Mzee mganga alitoka chumbani akaanza kusema:

“Huyu ndugu yenu ilitakiwa alale na jini aliye katika umbo la nyoka, ameogopa…

SONGA NAYO…

Nilimueleza yule mzee mganga jinsi nyoka aliyemlaza kitandani alivyoshuka, hivyo kunifanya mimi kutimka mle chumbani na nilipoona ule mfuko wa rambo ukipeperushwa na upepo nikaamini kuwa ni yule nyoka ananifuata ili aning’ate.

Maelezo hayo yaliwafanya kaka zangu, Ipacho na Bwana Makang’ako kuangua kicheko.

“Msicheke jamani, haya mambo ni mazito,” nilijitetea.

“Sasa mzee huyu bwana kulala na huyo nyoka hataweza, kwani hakuna mbadala wa hayo uliyoyaagiza?” aliuliza kaka Ipacho.

“Hakuna kisichowezekana, maadamu ameshindwa hilo tutatafuta njia nyingine,” alisema yule mzee huku akichukua mkebe wenye rangi nyeusi.

Alituamuru tutoke pale nje ya nyumba yake na kwenda kwenye kile chumba kilichokuwa na nyoka.

Hakuna kati yetu aliyekuwa tayari kuingia kwenye kile chumba.

“Mzee ingia kwanza wewe ili umtoe huyo nyoka,” nilisema mimi.

“Nyoka gani?” alihoji.

“Unauliza? Umeniacha na nyoka na ameshuka kitandani, unaulizaje swali hilo?”

“Nimekuambia hakuna nyoka, maana yake ni kwamba katoweka. Hakuna nyoka yule, alikuwa ni jini aliyekuwa kwenye umbo la nyoka!”

Aliingia ndani ya kile chumba na kwa kuwa kilikuwa na mwanga wa taa iliyokuwa ikiwaka kutokana na nguvu ya jua, mwanga ulikuwa mkali.

Baada ya mwenye nyumba kuingia nilifuatia kisha kaka zangu wakafuata. Kitu cha kwanza nilichokifanya baada ya kuingia ni kuwasha tochi ya kwenye simu yangu na kupiga magoti kisha kumulika chini ya uvungu wa kitanda.

Nilimulika kila kona licha ya kuwa na taa na kuthibitisha kuwa hakukuwa na nyoka mle chumbani kwani chumba chenyewe kilikuwa na mkeka mwekundu na kitanda chenye godoro ambacho hakikutandikwa shuka yoyote juu yake.

Nilipigwa na butwaa kuona hakukuwa na yule nyoka, moyoni nikajiambia kuwa huenda ni kweli alikuwa nyoka jini.

Yule mzee alitoka tena mle chumbani na kwenda nje baada ya dakika nne au tano hivi aliingia akiwa na njiwa mweupe, kumbe alikuwa na banda la njiwa nyuma ya nyumba yake kubwa.

Alimchinja.

“Basi tutoke na kesho tutakwenda kumtoa kaka yenu aliyewekwa msukule,” alisema yule mzee mganga.

Tulikuwa tumefika mjini Lilongwe Malawi, mzee mganga akasema hatuwezi kwenda kwa yule mwanamke aliyemfanya kaka Edgar zezeta bila kuwa na polisi.

“Unajua yule mama ananijua, akiniona tu tunaingia nyumbani kwake anaweza kutufanyia kitu kibaya sana. Anaweza akapiga kelele kwamba sisi ni wezi, tukamalizwa,” alishauri yule mganga.

Je, polisi watakubali kufuatana nao kwenda kumtoa kaka yao ambaye amewekwa msukule? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply