The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu -31

0

Yule mama alipewa kalamu, akasaini.

“Hapa mjumbe wenu ni nani?” aliuliza kamanda wa polisi wakati anaipokea ile hati iliyosainiwa.
“Ni nyumba ya tatu hapo kulia.”

“Lazima akaitwe ashuhudie upekuzi huu.”
“Sasa kosa ni nini?”
“Akaitwe kwanza huyo mjumbe ili naye asikie tunachokitafuta.” Nilitamani kujitokeza ili anione maana akiniona tu, atajua ni kwa nini polisi wanataka kumpekua. Alitumwa yule msichana wa kazi kwenda kumuita mjumbe.
Je, mjumbe atapatikana na itakuwaje? SONGA NAYO…

Hakuchukua muda mrefu, msichana yule alirudi akiwa ameongozana na baba wa makamo, mrefu mwembamba na alionekana kuwa ana busara kwa kumuangalia tu.

Mara baada ya kukutana na mkuu wa polisi wa upelelzi walianza kusalimiana:
“Bwana hujambo? Mimi ni mkuu wa upelelezi Inspekta Ben Mtwanga,” alisema yule mkuu wa polisi na jina hilo likanivuta katika hisia kwa sababu niliwahi kuwa na rafiki aliyekuwa akiitwa jina kama hilo lakini kwao ni Nachingwea. Hata hivyo, nikajisemea kimoyomoyo kwamba majina ya Kiafrika huwa yanafanana.
“Mimi naitwa Nico Namajani.”

“Bwana Namajani, unamfahamu mama huyu?”
“Ndiyo, namfahamu.”
“Unamfahamuje?”

“Namfahamu kama jirani yangu lakini pia kama mmoja wa watu wangu wa mtaa, mimi ni kiongozi wake.”
“Hilo jibu ndilo lililofanya tukutafute. Sisi tumekuja kumpekua na hii hapa hati ya kusachi nyumba yake na wewe ukiwa ni mjumbe wa mtaa huu, saini hapa,” alisema Inspekta Ben Mtwanga huku akiandika andika. Inawezekana alikuwa akiandika majibu ya yule bwana.

Yule mjumbe aliisaini karatasi ile kisha akawaangalia wale askari akahoji:
“Kwani mnamtuhumu nini?”
“Huyu mama analalamikiwa na watu kutoka nje ya nchi kwamba ana watu amewaweka humu ndani au nje ya nyumba hii lakini kwenye ua wake.”
“Nani analalamika?”

“Usiulize hilo. Sisi polisi tukipewa habari kama hiyo ni jukumu letu kuhakikisha madai hayo kama ni ya kweli au uongo.”
Yule mama ambaye ni shemeji yetu aliposikia hivyo akaanza kuweweseka huku akionesha kuwa hahusiki kuficha watu katika nyumba yake. Hakujua kuwa sisi tupo ndani ya gari kwani vioo ambavyo ni tinted vilifungwa na Bwana Makang’ako aliwasha kiyoyozi.

“Nani huyu aliyewaambia habari hiyo. Mimi nifiche mtu? Kwa faida gani. Afande hao watu ni maadui zangu tu kibiashara, usiwasikilize.” Alisema yule mama.
“Mama naomba usitufundishe kazi,” alisema kwa ukali kidogo yule Kamanda Ben Mtwanga na yule mama akaonekana kunywea.

Wote wakaingia ndani, ndipo mganga wetu naye akatoka haraka na kuungana nao. Yule mama hakumtambua kwa kuwa yule mzee mganga alikuwa amevaa kofia pana maarufu kama pama.
Waliingia chumba cha kwanza, hawakuona mtu, wakaingia chumba cha pili, huko nako hawakukuta mtu yeyote.
“Mama hiki chumba analala nani?” aliuliza Kamanda Ben Mtwanga.
“Usiniulize hivyo, kwani unataka kupanga?”

“Mama mimi niko kazini, sitanii, kwa nini unajibu kama utani?” alifoka yule kamanda.
Je, watampata kaka yao? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply