Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu – 34
ILIPOISHIA.
Yule mama hakumtambua kwa kuwa yule mzee mganga alikuwa amevaa kofia pana maarufu kama pama.
Waliingia chumba cha kwanza, hawakuona mtu, wakaingia chumba cha pili, huko nako hawakukuta mtu yeyote.
“Mama hiki chumba analala nani?” aliuliza Kamanda Ben Mtwanga.
“Usiniulize hivyo, kwani unataka kupanga?”
“Mama mimi niko kazini, sitanii, kwa nini unajibu kama utani?” alifoka Kamanda Mtwanga.
Je, watampata kaka yao?
SINGA NAYO…
Kamanda huyo aliyeonekana kuwa makini na kazi yake, aliangaza huku na kule, kisha akaandika katika daftari lake, sikujua alikuwa anaandika nini kwa sababu nilikuwa mbali.
“Mama unamfahamu huyu?” alisema Kamanda Mtwanga huku akinyoosha kidole kuelekea kwangu.
Yule mama baada ya kuniona alishituka na hakujibu swali.
“Mama unamfahamu huyu na yule?” akanyoosha kidole kuelekea kwa kaka Ipacho.
“Nawafahamu.”
“Unawafahamuje?”
“Ni shemeji zangu.”
“Shemeji zako kwa vipi? Fafanua.”
“Huyu mmoja anaitwa Jerome Ugonile ni ndugu na aliyekuwa mume wangu, Edgar Ugonile na mwenzake ni ndugu yao anaitwa Ipacho Mavaka.” Inspekta Matwanga akaandika.
“Huyo mume wako ambaye ni kaka yao yupo wapi? Mbona umesema aliyekuwa mume wako?”
“Alifariki dunia kama wiki tatu sasa zimepita.”
“Kweli?”
“Kweli kamanda nao wanajua.”
“Sasa kwa taarifa yako hawa ndiyo wametufanya tuje kwako leo. Wanadai ndugu yao yupo humuhumu kwenye nyumba yako, unasemaje?”
“Si kweli.”
“Kwa hiyo tutaendelea kupekua kila sehemu mpaka tujiridhishe kuwa kweli hakuna mtu huyo, sawa?”
Kimya.
“Mbona hujibu?”
“Nitajibu nini, pekueni.”
Kamanda Matwanga akaamuru stoo ifunguliwe, akafungua na akaamuru askari mmoja aingie ndani. Alikaa humo kwa dakika tatu au nne hivi.
“Mkuu hakuna mtu,” akasema.
Baada ya kupekua kila sehemu katika nyumba kubwa, hakuonekana mtu yeyote. Msafara ukahamia nyumba ya uani ambayo ilikuwa ndogo. Ni maalum kwa mfanyakazi. Ilipekuliwa na hakukutwa na mtu.
Moyo wangu ulianza kudunda kama vile nilikuwa nakimbizwa. Nilikuwa na mawazo mengi, niliwaza kuwa kama alimhamisha usiku si tutakuwa tumeumbuka?
Yule mganga wetu wakati upekuzi huo ukifanyika alikuwa ameshika tunguri ndogo sana mkononi mwake na watu wengine walikuwa hawajaiona, mimi nilimuona kwa kuwa alikuwa karibu yangu mara kwa mara.
“Sasa waungwana nyumba zote mbili ndugu yenu hayupo, mmeridhika kwamba hayupo hapa?”
“Hapana, sijaridhika.” Nilisema huku sauti yangu ikiwa kama vile inatetemeka. Mara baada ya kusema hivyo yule mwanamke alinitazama kwa jicho la hasira lakini hakutamka neno lolote.
“Hujaridhika, sasa tukusikilize, unataka tufanye nini?”
“Lile banda la mbwa hatujalikagua,” nikasema.
“Tangu lini mtu akakaa kwenye banda la mbwa?” Yule mwanamke akadakia huku mwili wake ukitetemeka.
“Lakini mama kwa nini unajitetea? Huyu ndiye mlalamikaji.” Kamanda Matwanga akawa kama anataka kugeuka, asiende kwenye banda.
Je, kaka yao atakuwa wapi? Fuatilia Jumanne ijayo.