The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu-38

0

“Huyu mgonjwa mmoja ni kaka wa huyu aliyeingia naye, anaitwa Jerome Ugonile, tumefanya mengi mpaka kufika hapa ofisini kwako, huyu mwingine simfahamu lakini nimeamua atibiwe hapahapa kwa gharama zangu, ndiyo ubinadamu. Jerome, huyu ni Dokta Pius Namahonga ni mwenyeji wa nyumbani Tanzania isipokuwa alichukuliwa na hospitali hii ya misheni baada ya kusifiwa sana kule nyumbani.”
SONGA NAYO…

“Nashukuru kukufahamu Dokta Namahonga, wewe ndiyo tumaini letu la kupona kwa wagonjwa wetu.”

“Jamani wagonjwa hawa nimewachunguza kiukweli wana hali mbaya sana, hasa huyu ndugu yetu, Edgar Ugonile,” alimpima tena kwa kusikiliza mapigo ya moyo wake kwa kifaa chao ambacho kitaalam wanakiita Stethoscopes.

Aliniangalia kwa jicho la huruma huku akitikisa kichwa, nikahisi labda anataka kuniambia kuwa kwa tatizo alilonalo kaka yangu na hatua aliyofikia, hawezi kupona tena.

Moyo ulikuwa ukinienda kwa kasi sana huku kwenye kichwa changu maneno yake ‘wana hali mbaya hasa huyu kaka yako’, yakijirudiarudia akilini mwangu nikawa najiuliza mbona hafafanui? Nimuulize au hajamaliza kutufahamisha? Nikaamua kwamba nimuulize maswali lakini kabla sijafungua mdomo akaendelea:

“Wagonjwa hawa tutawapa dawa za kuweka ubongo sawasawa, dawa zake zinafanana na zile ambazo tunawapa vichaa,” alisema huku akiandika kwenye kadi ya hospitali ya kaka ambayo ilikuwa ndani ya jalada ambalo lilifunguliwa pale mapokezi na lilikuwa limening’inizwa kitandani upande wa miguuni.

Baada ya kuandika alichokuwa anaandika alimgeukia yule mgonjwa mwingine. Kwake hakuwa na kazi kubwa ya kutoa ufafanuzi kwa mtu kwa sababu hakuwa na ndugu kwa wakati ule.

Aliandikaandika katika kadi ambayo ilikuwa kwenye jalada lake na akaamuru wote wawili wapelekwe kufanyiwa kipimo cha CT Scan.

“Hawa kwa kuwa wameathirika ubongo ni lazima wakapimwe kwenye CT Scan ili tuone ubongo wao ukoje au umeathirika kiasi gani,” alituambia huku akimuelekeza mambo fulani nesi aliyekuwa karibu naye.

Hata hivyo, alimwambia yule nesi amfuate ndipo waliongozana kwenda katika chumba cha daktari ambako sikujua walikwenda kuongea nini.

Baada ya dakika kama nne walirudi walipotuacha kisha Dokta Namahonga akasema;
“Mtafuatana na huyu nesi, atawahudumia, mkipata majibu ya vipimo mtakuja kuniona tena,” alisema Dokta Namahonga.

Wagonjwa walitolewa kwenye chumba cha daktari na wakawekwa kwenye chumba cha mapumziko ingawa mlangoni waliandika ‘Observation.’

Haraka sana yule nesi alitoweka ile sehemu na kutokomea nisikokujua.
“Nisubirini dakika chache na poleni,” alisema nesi huyo na kumuacha mwenzake akiwaangalia wagonjwa wetu.

Lakini baada ya dakika tatu alirudi akiwa na chupa mbili za maji yaani drip na mirija yake pamoja na sindano na kipima sukari kilichoandikwa Gluco Plus. Aliwapima sukari yao kwenye damu.

“Wote sukari yao ipo sawasawa,” alisema kisha akawatundikia drip kila mmoja na kuburuza kitanda chao cha magurudumu akisaidiwa na yule nesi mwingine huku akituambia:
“Nifuateni.”

Tuliongozana nao hadi sehemu iliyoandikwa kwa juu mlangoni CT Scan Room. Tuliingia ndani lakini kulikuwa na sehemu ambayo kulikuwa na viti vinne. Tuliambiwa na yule nesi tuliyekabidhiwa na Dokta Namahonga tuketi hapo. Niliketi mimi na Bwana Makang’ako.

Mbele ya chumba hicho tulichoketi niliona kuna taa nyekundu inawaka na kwenye mlango wa kioo kumeandika: ‘Usiingie huku ila kwa tuhusa maalum.’

Tulikuwa tumebaki kimyaa huku kila mmoja akiwaza lake. Sikujua mwenzangu Bwana Makang’ako alikuwa anawaza nini lakini mimi niliwaza kwa wazazi. Nilikuwa sijawapigia simu kuwaeleza lolote kuhusiana na kaka maana wao waliamini kuwa ameshafariki dunia kutokana na taarifa ya awali ambayo alituletea yule mama ambaye sasa anashikiliwa na polisi.

Simu ya bwana Makang’ato iliita.
“Ni Inspekta Ben Mtwanga. Bila shaka ameona tumechelewa sana kutoka,” alisema.
“Pokea msikilize anasema nini.”

Huyu mzee aliweka spika ya nje akaanza kuzungumza naye.
“Haloo kamanda.”

“Sasa mzee mimi nampeleka huyu mama tunayemshikilia kituoni. Mkimaliza kuwahudumia na kuwalaza hao wagonjwa wenu, mje kituoni tuelekezane cha kufanya zaidi,” alisema Kamanda Ben Mtwanga.
“Sawa.”

Nilisikia ving’ora vikilia na nikajua kuwa ni yale magari ya polisi. Ndani ya chumba ambacho tuliketi kulikuwa na runinga na ghafla kukawa na taarifa ya kushtua (breaking news).
“Mwanamke anayedaiwa kufanya wanaume zezeta akamatwa,” alisema mtangazaji mmoja wa MTV kisha ukafuatia muziki uliopigwa kidogo, yule mtangazaji akaendelea:
“Mwanamke mmoja amekamatwa akiwa na wanaume wawili aliokuwa amewafungia kwenye banda la mbwa wake.

“Wanaume hao wamedhoofu na hali zao kiafya ni mbaya sana, hadi tunapotoa taarifa hii, wamepelekwa Hospitali ya Malamulo kwa matibabu. Tutaendelea kuwapasha habari hii baadaye,” alimaliza mtangazaji huyo.

Wakati habari hiyo inatangazwa kulipitishwa picha za wagonjwa kaka na yule mgonjwa mwingine, Banda Babali pamoja na watu waliofurika katika nyumba ya yule mama.
Nilishtuka baada ya kusikia sauti ya yule nesi akisema:

“Tayari turudi kwa daktari.” Alisema huku akiburuza kile kitanda chenye mgonjwa wangu.

Tulifika ofisini kwa Dokta Namahonga naye akachukua yale majalada ya wagonjwa.
Akianzia kulisoma lile la kaka; alitikisa kichwa wakati anachunguza zile picha zilizopigwa na CT Scan. Alinichanganya tena.
“Je, hawawezi kupona?” nilijiuliza.
Usikose kusoma muendelezo wa simulizi hii wiki ijayo.

Leave A Reply