The House of Favourite Newspapers

Mama Aliyedhalilishwa Akijifungua Kulipwa Sh. Milioni 56.5

MAHAKAMA Kuu nchini Kenya imeamuru mwanamke aliyeteswa na kudhalilishwa wakati wa kujifungua hospitalini, Josephine Majani, alipwe fidia ya dola 25,000 (Tsh. Milioni 56.5).

 

Tukio la Josephine kudhalilishwa lilitendeka mwaka 2013 katika Hospitali ya Bungoma, Magharibi mwa Kenya ambapo kisa hicho kilizua maswali na mijadala kutoka kwa raia na wanaharakati watetezi wa haki za Binadamu baada ya kusambaa kwenye vyombo vya habari na mtandaoni.

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Bungoma, Abida Aroni, alisema MamlAka ya Afya nchini humo ilikiuka haki za kimsingi za Josephine Majani alipotengwa na kukosa kuhudumiwa wakati wa kujifungua katika hosipitali ya umma mwaka 2013.

Jaji huyo alisema kuwa haki za msingi za afya za Josephine, pamoja na heshima yake vilikiukwa kupitia kuteswa kimwili na kutukanwa na wauguzi katika hospitali ya Bungoma hivyo kutokana na hilo, akaamuru alipwe fidia  hiyo.

 

Josephine amesema amefurahia uamuzi huo akisema kuwa hatimaye haki imetendeka baada ya mtu kurekodi video kwenye simu yake na kuipakia kwenye mtandao wa kijamii huku akisema fidia hiyo itamsaidia kumlea mtoto ambaye karibu ampoteze wakati wa kujifungua.

 

Martin Onyango, wakili wa Josphine kutoka kituo cha Afrika kuhusu afya ya uzazi anasema huo ni ushindi mkubwa kwa wanawake wanaotafuta huduma bora za afya ya uzazi katika hospitali za umma nchini Kenya.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu, wanawake 495 kati ya laki moja walio wajawazito hufa kila mwaka kutokana na matatizo wakati wa kujifungua.

Comments are closed.