The House of Favourite Newspapers

MWANAMKE AMUOA MWANAMKE MWENZAKE BONGO

MARA: UKISTAAJABU ya Musa, utayoona ya firauni! Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Ninyangi Sedeki (50), mkazi wa Kijiji cha Kerende, Kata ya Kemambo wilayani Tarime Vijijini, amekiri kumuoa mwanamke mwenzake na kufanikiwa kupata ‘watoto’ wawili, wa kiume na wa kike.

Akizungumza na Uwazi hivi karibuni, mwanamke huyo alisema, akiwa katika Kitongoji cha Malera aliolewa na mwanaume wake na kuanza maisha lakini hakufanikiwa kupata mtoto wa kiume hadi mwanaume huyo alipofariki.

“Kwa miaka mingi sikufanikiwa kupata mtoto wa kiume, nilikuwa nazaa wa kike tu, siku zinavyozidi kukatika umri nao unasogea na watoto wa kike wakaolewa nikawa sina mtoto hapa nyumbani,” alisema mama huyo. Alisema katika mila na desturi za kabila lao kama hukuweza kupata mtoto wa kiume au alimpata lakini alifariki au hukumpata kabisa, inabidi familia yake iendelee kuomba jina la ukoo wake.

“Baada ya kuruhusiwa kutumia jina la ukoo, inakupasa sasa utafute binti ambaye atakubaliana na wewe kuwa aje kuwa mbadala wa mtoto wako yaani mkamwana wako. “Binti huyo akikubali, unamtolea mahari na sherehe hufanywa baada ya hapo huwa ni uamuzi wake kuchangua ni mwanaume yupi ataweza kuzaa naye,” alifafanua mama huyo.

Alisema binti huyo akifanikiwa kuzaa mtoto wa kiume, basi ndiye ambaye atarithi mali ya familia kwa mujibu wa mila na desturi za Wakurya. Alifafanua kuwa watoto watakaozaliwa wote na mwanamke aliyeolewa na mwanamke mwenzake majina ya ukoo ya watoto yatatumika ya ‘mumewe’ yaani mwanamke aliyeoa.

Hata hivyo, mama huyo alisema kadiri siku zinavyokatika ndivyo mila hiyo inavyozidi kufa kwa kuwa wasichana wengi wa siku hizi, hawakubali ndoa hizo maarufu kwa jina la Ntobu.

“Siku hizi wasichana wengi hawapendi kuolewa na wanawake wenzao kutokana na kupata elimu. Lakini wengi wanaokubali siku hizi ni wale wasichana ambao huzalishwa wakiwa nyumbani kabla ya kuolewa,” alisema mama huyo.

Alipoulizwa kwa nini wasichana waliozalishwa wakiwa kwao huolewa na wanawake wenzao mama huyo alisema ni kwa kuwa kimila, wanakuwa hawana heshima kama wale ambao hupata wachumba wakaolewa wakazaa wakiwa ndani ya ndoa.

Mama huyo alisema yeye alioa msichana ambaye alifanikiwa kuishi naye kwa miaka sita lakini akafariki dunia na kumuachia watoto wawili mmoja wa kiume na mwingine wa kike hivyo anaishi maisha ya kawaida na yenye faraja kwani ana wajukuu na anadahi hata akifa leo hii familia yake itaendelea kuwepo na amepata warithi.

Mbali na mwanamke huyo, Uwazi lilibaini uwepo wa mwanamke mwingine katika kijiji hichohicho aitwaye Anastazia ambaye aliolewa ndoa ya Ntobi lakini hakutaka kueleza kwa undani kuhusu ndoa yake hiyo. Uchunguzi zaidi uliofanywa na Uwazi umebaini kwamba baadhi ya makabila mkoani Mara bado wanawake wanawaoa wanawake wenzao.

Tabia hiyo ambayo kwa mujibu wa Wakurya, ni jadi yao na ni huwa ni mila na desturi zao walizorithi kutoka kwa mababu zao.

Akizungumza na gazeti hili, mzee mmoja wa Kikurya, John Paul alikiri kwamba wanawake wanaruhusiwa kuoa wanawake wenzao kwa sababu maalumu. “Katika kabila la Wakurya tumegawanyika kwani kuna makabila madogomadogo kama vile Wachari, Wakira, Warechoka, Watimbalu, Wanyabasi Warege na kadhalika.

“Wote hawa mila hufanana ila huishi kwa kugawanyika sehemu tofautitofauti mkoani Mara. Wote hawa mwanamke anaweza kuoa mwanamke mwenzake,” alisema mzee Paul. Akizungumzia tamaduni hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Mniko Magabe alisema ndoa hizo kwa kabila la Kikurya ni moja ya mila na desturi za tangu ukuaji wake yeye alikuwa anaona.

“Ni jambo linalofanywa tangu enzi za mababu hadi leo nayaona japokuwa siku hizi watu wamebadilika na matukio kama hayo yanaendelea kupungua kadiri siku zinavyozidi kwenda kutokana na watu kuelimika, wanazidi kupata elimu,” alisema kiongozi huyo.

Matukio kama hayo ya mwanamke kuona mwanamke mwenzake hayakuzoeleka kutokea hapa nchini na badala yake Watanzania walikuwa wakiyasikia yakifanyika nje ya nchi kama vile Afrika Kusini.

Katika nchi hiyo tukio lililovuma sana ni la Anele Mkuzo aliyeolewa na Seipati Magape waliofunga ndoa mwaka juzi katika Jimbo la Gauteng na kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii hasa waliposema kwamba wanatarajia kuzaa watoto wengi ikiwezekana waunde timu ya mpira wa miguu.

STORI: NELSON BONZO, UWAZI

Comments are closed.