The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Jini Alivyonipenda na Kunipeleka Ujinini! – 3

0

ILIPOISHIA JUMATATU

Siku moja nilialikwa kwenye harusi ya rafiki yangu mmoja aliyekuwa akiishi wilayani Mkinga.

Nikaenda kuazima gari kwa rafiki yangu Martin ili niweze kuhudhuria harusi hiyo.

Niliondoka Tanga saa nne asubuhi nikafika Mkinga saa tano na nusu.  Ndoa ilifungwa saa saba mchana.  Baada ya  kufungwa kwa ndoa hiyo sherehe ziliendelea hadi usiku.

NIKIWA kwenye sherehe hizo nilikutana na msichana mmoja ambaye nilikuwa simfahamu lakini alinisalimia kwa uchangamfu kama aliyekuwa akinifahamu.  Alikuwa amevaa baibui la Iran.  Alikuwa mweupe kama Mwarabu na alikuwa na lafudhi ya ki-Mombasa.

Sikuweza kukumbuka kama nilikuwa namfahamu yule msichana au la.  Na pia sikuweza kukumbuka kama niliwahi kukutana naye mahali.  Ilipofika saa saba nikaamua kuondoka.  Niliwasha gari nikaanza safari ya kurudi Tanga.

Kabla ya kufika eneo liloitwa Mabokweni, gari likazimika ghafla.  Lilizimika katikati ya msitu uliokuwa unatisha kwa giza.  Nikajaribu kuliwasha gari hilo lakini halikuwaka.

Nikataka kushuka ili nikafungue boneti la mbele nijaribu kuchokonoa mashine lakini niliogopa.  Pale mahali palikuwa ni kwenye msitu.  Nilihisi ningeweza kushambuliwa na wanyama au kitu chochote.

Nikabaki ndani ya gari huku moyo wangu ukiwa umejaa hofu.  Nilikuwa nikiwaza nitaendelea kubaki pale hadi muda gani kwani gari ndiyo lilikuwa limeshanigomea.

Taa za mbele za gari zilikuwa zinawaka.  Ghafla nikaona kitu kama mtu mrefu anavuka barabara akiwa umbali wa kama mita ishirini mbele yangu.  Alitokea upande wa kushoto wa barabara akapotelea kwenye msitu upande wa kulia.

Tukio lile lilinishitua sana.  Moyo wangu ukawa unakwenda mbio.  Nikajiambia kimoyomoyo: “Kumbe mahali hapa ni pabaya!  Ni kitu gani kile nilichokiona?

Kile kitu kilichopita kwanza kilifanana na binadamu mrefu kilikuwa na umbile la mwanamke.  Baada ya kama dakika moja hivi kikapita kiumbe kingine kirefu kama kile cha kwanza kilichokuwa na umbile la mwanamme!

Kiumbe hicho kikamulikwa na taa za gari lingine lililokuwa linakuja nyuma yangu.  Kilipoona mwanga unaongezeka  kilitokomea haraka kwenye msitu.

Nikageuka nyuma kulitazama gari lililokuwa linakuja.  Kutokana na mwanga wa taa wa gari hilo sikuweza kuliona lilikuwa gari dogo au lori.  Hata hivyo, kutokea kwa gari hilo kukanipa matumaini ya kupata msaada.

Nikafungua mlango wa gari kwa haraka nikashuka na kuanza kulipungia mkono.  Sikuwa  na hakika kama lingesimama kwani madereva wengi wa magari wamekuwa waoga kusimamisha magari porini wakati wa usiku kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ujambazi.

Gari hilo ambalo halikuwa likienda kwa mwendo wa kasi sana lilipunguza mwendo na kunipita.  Nikaliona lilikuwa Land Cruiser jipya la muundo mpya wa kisasa.  Nikadhani lisingesimama.  Ghafla lilipunguza mwendo tena likaelekea pembeni mwa barabara na kusimama.

Nilishukuru sana.  Nikatembea harakaharaka kulifuata.  Nilipoufikia mlango wa dereva aliyekuwa akiliendesha nikaona alikuwa mwanamke, tena alikuwa peke yake.  Lakini kitu ambacho sikukitarajia, mwanamke mwenyewe alikuwa ni yule niliyekutana naye kwenye sherehe ya harusi ya rafiki yangu.

Aliponiona akashangaa.

“Kumbe ni wewe?” akaniuliza.

“Ni mimi.  Natumaini tulikutana kwenye harusi.”

“Ndiyo, tulikuwa pamoja, kumbe ulitangulia kuondoka!”

“Niliwahi kuondoka lakini gari langu limeharibika, nilikuwa nahitaji msaada wako.”

Bila kutarajia, msichana yule alifungua mlango akashuka.  Kitendo kile kilinifanya nimuone alikuwa msichana jasiri sana.

“Limeharibika kitu gani?” akaniuliza.

“Sijui.  Lilikata moto ghafla tu.”

Nilimjibu yule msichana lakini sikuwa na amani.  Macho yangu yalikuwa kwenye ule msitu pale walipoingia wale watu warefu.  Nilihofia wasije wakatokea tena na kutushambulia.

“Hebu twende,” msichana yule akaniambia.

Tukaenda kwenye lile gari.  Msichana alikuwa na hatua kama mwanamme!  Tulipolifikia gari hilo aliniambia:

“Hebu ingia ujaribu kuliwasha tena.”

Nikafungua mlango wa gari na kuingia.  Nikajaribu kuliwasha bila mafanikio.

“Mafuta yamo?” msichana akaniuliza.

“”Nilitia ya kutosha.”

“Sawa itakuwaje?”

“Kama itawezekana, ningekuomba unisaidie kulivuta hili gari.  Nikiliacha hapa linaweza kuibiwa.”

“Sawa, nitakuvuta.”

“Nitakushukuru sana dada yangu.”

Msichana alirudi kwenye gari lake akalirudisha kinyumenyume hadi likakaribia nilikoliegesha like gari.  Akashuka na kuchokonoa kamba ya chuma iliyokuwa nyuma ya gari lake.  Tukasaidiana kulifunga gari langu.

Je, nini kiliendelea? Fuatilia hapahapa Ijumaa.

Na Faki A. Faki

====

Usipitwe na Matukio, Download na Install ==> Global Publishers App

Daktari Achezea Kipigo Baada ya Kubambwa LIVE Akipokea Rushwa

Leave A Reply