MWANAMKE MBARONI MAUAJI YA MJESHI!

KIMEWAKA ile mbaya! Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limefanya msako mkali kisha kuwatia mbaroni watuhumiwa kadhaa akiwepo mwanamke mmoja kwa tuhuma za mauaji ya mwanajeshi au mjeshi, Gazeti la Ijumaa Wikienda lina kisa na mkasa.  Jeshi hilo lilimtia mbaroni mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Neema Ally Kibwana na kuunganishwa na watuhumiwa wengine tisa kwa tuhuma hizo.

MAUAJI YA MJESHI

Neema na wenzake wanatuhumiwa kwa mauaji ya askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), SSGT Leonard Lwimba wa Kambi ya Pangawe katika Manispaa ya Morogoro. Mauaji hayo yalijiri hivi karibuni nyuma ya Uwanja wa Maonesho ya Nanenane kwenye mashamba ya mkongwe kuelekea kiwanda cha mkonge cha Tungi mjini hapa.

MASHUHUDA WA TUKIO

Wakizungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda, mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Kasim Saleh Dilunga alisema; “Unajua kwa sasa hapa Morogoro kuna wizi wa bodaboda ambao umeshamiri, tunasikia matajiri wa kununua hizo bodaboda za wizi wapo Dumila mkoani hapa na Chalinze mkoani Pwani.

“Huyu mjeshi alikuwa amevaa kiraia akiwa na pikipiki yake, hatujui mazingira aliyokutana na hao wezi yalikuwaje kwa kuwa hakukuwa bodaboda, lakini walichomfanyia ni unyama wa kutisha. “Inasemekana walimtaiti kisha wakampiga mapanga, wakamuua na kumpora pikipiki yake. “Katika kupoteza ushahidi ndipo wakamtupa kwenye mashamba ya mkonge nyuma ya Uwanja wa Nanenane njia ya kuelekea Tungi.

“Alitafutwa sana na familia yake pamoja na wanajeshi wenzake hadi walipofanikiwa kumpata siku mbili mbele kwenye mashamba ya mkonge huku mwili wake ukiwa umeharibika kutokana na kukatwakatwa na mapanga.”

Kwa upande wa bosi wa zamani marehemu Leonard, Captain John Mahayo alipotakiwa kumuelezea marehemu alikuwa na haya ya kusema;

“Kama unavyojua kabla mimi sijastaafu jeshi nikiwa na cheo cha captain nilikuwa visiwani Zanzibar kwenye Kambi ya Bavuai 12 KJ. Marehemu Leonard nilikuwa naye akiwa chini yangu kabla ya kuhamishwa mwaka 1998 kuja Kambi ya Pangawe hapa Morogoro.

“Kambi ya Pangawe ameitumikia kwa muda mrefu mpaka umauti unamkuta kwa kuuawa na majambazi kwenye mashamba ya mkonge ya Tungi.“Kimsingi marehemu alikuwa na nidhamu ya hali ya juu kikosini. Binafsi kifo chake kimeniuma sana kama mtu niliyemfahamu vizuri.”

KAMANDA MUTAFUNGWA

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Wilbrord Mutafungwa alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuwashikilia watuhumiwa hao akiwemo Neema. “Tunawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kumuua Leonard ambaye ni mwanajeshi wa Kambi ya Pangawe hapa Morogoro.

“Kati ya watuhumiwa hao yupo mwanamke huyu aliyeunganishwa kwenye kesi hiyo baada ya kukutwa na simu ya marehemu. “Upelelezi umekamilika na  leo (ljumaa) tunawapeleka mahakamani watuhumiwa hao,” alisema kamanda huyo anayesifika kwa uchapaji kazi mzuri mkoani hapa.

Ijumaa majira ya saa 5:00 asubuhi watuhumiwa hao walitolewa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Morogoro na kupelekwa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro chini ya ulinzi mkali wa magari matatu ya polisi ambayo yalikuwa yamejaa askari wenye silaha za moto pamoja na pikipiki mbili za polisi.

AZUA MSHANGAO

Neema ambaye ni mwanamke pekee aliyekuwa miongoni mwa watuhumiwa hao huku wengine wakiwa ni wanaume, alizua mshangao kwa kuwa ni mara chache mno wanawake kuonekana kwenye tuhuma nzito kama hizo.


Loading...

Toa comment