Mwanamke Mwingereza Aliyejiunga ISIS Aomba Kurejea Nchini

BAADA ya kuvuliwa uraia wake wa Uingereza, Shamima Begum (pichani) aliyejipatia umaarufu wa ghafla dunia nzima, ameipigia magoti nchi yake hiyo kuomba imrudishie uraia wake kwa kusema hatamani tena kuishi nchini Syria ambako alikimbilia kujiunga na wapiganaji wa Kiislam (ISIS) au kundi linalojipambanua kuwa na misimamo mikali ya dini ya Kiislamu. 

Mwaka 2015 Shamima na wenziye wawili, Amira Abase na Kadiza Sultana, wakiwa na umri wa miaka 15 – 16  na wote wakiwa raia wa Uingereza wa kuzaliwa nchini humo, walikuwa wanafunzi wa sekondari  ya Bethnal Green Academy, wakati wa likizo walikimbilia nchini Syria kupitia Uturuki ili wakajiunge na ISIS.

Walipofika wote waliolewa na wapiganaji wa kundi hilo linalohusishwa na mambo ya kigaidi.  Shamima katika umri huo mdogo alizalishwa watoto watatu ambapo wawili wamefariki kwa ugonjwa ambao hakuujua pamoja na utapiamlo kwa mujibu wake mwenyewe.

Amesema huduma za kiafya ni mbovu. Wenzake  hao wawili pamoja na waume zao hao wapiganaji wanadaiwa kufariki katika mapigano. Ndugu wa wenziye hao wawili wamekata tamaa kuwaona tena ingawa Shamima anasema amesikia mmoja wao yupo hai kwenye makambi ya Syria ila mawasiliano hawana.

Wiki kadhaa zilizopita Shamima akiwa Syria kwenye makambi ya wakimbizi ameweza kuzungumza na vyombo vikubwa vya habari na anachoiomba Uingereza imsamehe ili arudi nchini mwake humo yeye na mwanaye aliyemzaa mwezi Februari mwaka huu.

Amesema tangu azungumze na vyombo vya habari, uhai wake umezidi kuwa hatarini kwani wanawake wenzake  wapiganaji wanamtishia kumuua. Uingereza imekataa kumrudishia uraia ikisema kuna tishio kwani Shamima anaweza akawa hatari kwenye usalama wa taifa hilo na raia wake na wao Uingereza hawana kosa kwa kuwa alikimbia mwenyewe, wakidai yamemkuta aliyoyataka.

Yago, 29, Jamaa aliyemuoa Shamima ambaye naye alikuwa mpiganaji wa ISIS kabla ya kujisalimisha upande wa pili wa Syrian Democratic Forces, sasa ni mateka.  Yeye ni raia wa Uholanzi na akirudi nchini mwake anakabiliwa na kifungo cha miaka sita jela kwa kujiunga na kikundi kinachotajwa kwa ugaidi.

Yago,  kwa mujibu wa Aljazeera,  kupitia shirika la habri la Uingereza (BBC), amesema yeye na Shamima wanaweza kwenda kuishi nchini Uholanzi kwa kuwa na yeye hataki tena kuendelea na mambo ya ISIS na kundi hilo linamuona kama msaliti na walimsulubu sana.

Shamima amesema yeye alikuwa mke tu hakujihusisha na mauaji au vitendo vingine vya kigaidi kama wengine. Mumewe huyo amesema anamuonea huruma mkewe na mtoto wao lakini pia anasema taifa lolote ikiwemo Uingereza lazima liwe na hofu kuhusu usalama wa raia wake.

Licha ya kuzaliwa Uingereza na kusoma huko, wazazi wa Shamima wana asili ya Bangladesh.   Ali Ahmed baba mzazi wa Shamima kwa sasa anaishi Bangladesh na mke wake wa pili, alipohojiwa amesema anaiomba Uingereza imsaidie mwanaye arudi salama kwa  kuwa anaamini alishawishiwa kuondoka Uingereza kujiunga na ISIS na hata akili zake zilikuwa bado za kitoto. Bangladesh imekataa kumpa uraia Shamima ikisema ni mtu wa Uingereza hivyo Uingereza isiwatupie mzigo usiowahusu

Loading...

Toa comment