Mpenzi msomaji wangu ni Jumatatu nyingine murua tunakutana tena kwenye safu yetu hii ya XXLove kwa ajili ya kupeana elimu juu ya uhusiano. Kichwa cha mada yetu ya leo ni msemo uliozoeleka mitaani ukimaanisha kuwa mwanamke siyo umbo na urembo bali ‘kinachomata’ ni tabia.
Inawezekana msemo huo ukawa sawa au usiwe sawa ila lengo ni ujumbe uwafikie walengwa.
Ninaamini kabisa wewe msomaji ni shuhuda kwa namna ambavyo Mungu amekujalia sura yenye mvuto, figa bomba na kadhalika lakini hadi sasa unaelekea kuzeeka, hujaolewa au hujapata mchumba wala mtu wa kukutamkia kuwa yuko tayari kukuweka ndani uwe mkewe, unadhani ni kwa nini?
Inawezekana tabia yako haiendani na uzuri wako, kila anayetaka kukuoa, akikuangalia kwa sura na umbo, anakuona upo vizuri lakini akija kwenye tabia na vitu vingine vya ziada, anakuta hakuna kitu, hicho ndicho kinachokuponza kuendelea kugeuzwa ‘shamba la bibi’ na kukosa mwanaume wa kukuoa. Kumbuka kuwa ndoa inakujengea heshima katika jamii.
Sehemu kubwa ya waoaji hupendelea mtu atakayekuwa tayari kuepukana na mambo ya kimjinimjini (usistaduu na umapepe). Hawapendi mwanamke ambaye kila siku anawaza kwenda klabu. Kila wikiendi anashinda baa kwenye viti virefu akipata kilaji. Hata kama unakunywa, si unywe kistaarabu au uache kabisa ama ununue ukanywee nyumbani?
Mwanaume anahitaji mwanamke anayejitambua, mwenye utayari wa kubadilika kifikra kutoka kwenye usistaduu na kuwa mama wa familia.
Unapaswa kufahamu kuwa muoaji anahitaji mchumba ambaye yuko tayari kukabiliana na hali zote kwa maana ya shida na raha, lakini kila mtu akikutazama anakuona huwezi kuishi kama mama wa familia, ujana mwingi, ujuaji na uzuri wako vinakufanya ujione kama umeshushwa kutoka mbinguni hasa ukiongezea na elimu kidogo ya chuo inayokupa mshahara, hilo ndilo tatizo linalowaponza wengi.
Mpenzi msomaji kama wewe ni mlengwa wa makala haya unapaswa kukaa chini, ujiulize ni kwa nini umejaliwa ulivyojaliwa lakini hujapata mchumba wala hujaolewa na hadi sasa unaishi kwenu?
Ukishaufahamu udhaifu wako, basi jitahidi kuurekebisha haraka iwezekanavyo la sivyo utaendelea kusota ukiwa ‘singo’ hadi uzeekee nyumbani kwenu au kwenye mageto ya wanawake wa mjini.
Kwa maoni na ushauri, tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mitandao ya Kijamii ya Facebook, Insta:@mimi_na_uhusiano au unaweza kujiunga kwenye group letu la WhatsApp kwa mijadala na elimu zaidi.
@@@