The House of Favourite Newspapers

Mwanamuziki Kunyongwa kwa Kumkufuru Mtume

0

MWANAMUZIKI anayetambulika kwa jina la Yahaya Sharif-Aminu, mwenye umri wa miaka 22, kutoka  Jimbo la Kaskazini mwa Nigeria la Kano amehukumiwa kifo kwa kumkufuru Mtume Muhammad (SAW).

 

Mahakama ya Kuu ya Kiislamu inayotumia Sharia katika eneo la Hausawa Filin Hockey katika jimbo la Kano imesema kuwa Yahaya alipatikana na hatia ya kukufuru kwa wimbo wake uliosambazwa kupitia mtandao wa WhatsApp mwezi Machi lakini alikanusha mashtaka hayo.

 

Jaji Khadi Aliyu Muhammad Kani alisema kuwa anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo dhidi yake. Majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria yanayokaliwa na Waislamu wengi hutumia sheria ya Kiislamu na sheria ya kawaida, ambayo haitumiwi kwa watu ambao sio wafuasi wa dini ya Kiislamu.

 

Ni moja tu ya hukumu za kifo zilizopitishwa na mahakama za sheria nchini Nigeria tangu zilipoanzishwa mwaka 1999. Mwanamuziki huyo ambaye kwa sasa anashikiliwa mahabusu, alikuwa amejificha baada ya kutunga wimbo huo.

 

Waandamanaji walichoma moto nyumba ya familia yake na kukusanyika nje ya makao makuu ya polisi ya Kiislamu huku Hisbah wakidai hatua ichukuliwe dhidi yake. Wakosoaji wanasema wimbo ulikufuru kwani ulimsifu imam kutoka Waislam wa Tijaniya kiasi kwamba ulimpatia hadhi ya juu kuliko Mtume Muhammad.

 

Kiongozi wa maandamano hayo, Idris Ibrahim, alidai kukamatwa kwa mwanamuziki huyo mwezi Machi,  hukumu itakuwa kama onyo kwa wengine “wanaojaribu kufuata nyayo za Yahaya”.

“Niliposikia kuhusu hukumu nilifurahi sana kwa sababu inaonyesha kuwa maandamano yetu hayakuwa ya bure. Hukumu hii itakuwa mfano kwa wale ambao wanahisi kuwa wanaweza kutukana dini yetu au mtume na waendelee kuwa huru,” alisema.

Yahaya Sharif-Aminu ni nani?
Mwimbaji huyo wa nyimbo za dini ya Kiislamu, hakufahamika sana kaskazini mwa Nigeria na nyimbo zake hazikuwa maarufu nje ya madhehebu yake ya Tjjaniya, kwani kuna wanamuziki wengi wanaoimba kwa kiwango kama chake.

 

Hukumu kadhaa zimekuwa zikipitishwa, ikiwemo dhidi ya wanawake wanaopatikana na hatia ya kufanya ngono nje ya ndoa. Lakini ni hukumu moja tu ambayo imewahi kutekelezwa dhidi ya mwanamme aliyepatikana na hatia ya kumuua mwanamke na watoto wake wawili ambao waliuawa kwa kunyongwa mwaka 2002.

 

Mara ya mwisho mahakama ya sheria ya Nigeria kutoa hukumu ya kifo ilikuwa ni mwaka 2016 wakati Abdulazeez Inyass, alipohukumiwa kifo kwa kukufuru dini ya Kiisalmu baada ya kuendeshwa kwa kesi ya siri katika jimbo la Kano.

 

Inadaiwa kuwa mtu huyo alisema kwamba Sheikh Msenegal Ibrahim Niasse, muasisi wa madhehebu ya Tijaniya, ambayo yana wafuasi wengi  Afrika Magharibi  “ni mkubwa kuliko Mtume Muhammad”.

 

Hukumu haijatekelezwa kwani adhabu ya kifo inahitaji kuidhinishwa kwa saini ya gavana wa jimbo.

Leave A Reply