BAADA Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, kushughulikia kero mbalimbali za migogoro ya ardhi na kutolea ufumbuzi, tatizo hilo bado linaendelea kwa baadhi ya watu ambao wanaenda kinyume na taratibu zilizopo.
Hayo yamebainika baada ya mwananchi mmoja anayefahamika kwa jina la Ally Abdallah ambaye ni mmiliki wa kiwanja namba 212 kilichopo Kinondoni, Mkwajuni, kujitokeza mbele ya vyombo vya habari kulalamikia kuwa nyumba yake imetapeliwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Suleiman ambaye naye amekuwa akidai ni mmiliki halali wa kiwanja hicho
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ally alisema kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa eneo hilo na akaonyesha nyaraka mbalimbali kwa waandishi wa habari za barua ambazo alipewa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam zinazoonyesha kuwa namba ya kiwanja anayoitumia inampa uhalali kuwa yeye ndiye mmiliki wa eneo hilo.
Baada ya maelezo hayo waandishi wa habari walizungumza na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kinondoni, Mussa Embe, ambaye alikiri kuufahamu mgogoro huo na kusema kuwa yeye anatambua eneo lake halina kiwanja namba 1200 kama mlalamikiwa anavyodai na badala yake eneo la kiwanja chake mwisho ni 429.
Abdallah amemwomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi na Mkuu wa Mkoa kuingilia kati mgogoro huo ili haki ipatikane.
Comments are closed.