MWANARIADHA ATOWEKA SIKU 240

DAR ES SALAAM: Mwanariadha maarufu ambaye alishiriki mbio za marathon mwaka 2017/18 Mtwara na kushinda, Denis Mathias (pichani) mkazi wa Tabata, Dar ametoweka katika mazingira ya kutatanisha huku madai ya kutekwa na kuuawa yakitawala.  

 

Akizungumza na Uwazi kaka wa mwanariadha huyo, George Mathias alisema Denis alitoweka Juni 2, 2018 ambapo ni takribani siku 240 zimepita.

 

Ilidaia kuwa, Denis akiwa na wafanyakazi wenzake wakitokea Morogoro kikazi alishuka Kimara Korogwe jijini Dar na kuwaambia kwamba anakwenda kukutana na mchumba wake kwanza kabla ya kuelekea nyumbani kwake, Tabata alikokuwa akiishi na baba yake ambaye ni mgonjwa.

 

“Wafanyakazi wenzake wanasema kuwa Denis alishuka hapo Kimara Korogwe muda wa saa nne usiku kwa maelezo kwamba anakwenda kuonana na mchumba wake.

“Kwa kuwa alikuwa anaishi na baba ambaye ni mgonjwa alimpa taarifa kwamba yuko njiani anarudi hivyo wakawa wanawasiliana lakini ilipofika saa sita usiku, mawasiliano yakakata na simu yake haikupatikana tena hewani mpaka leo.

 

“Kesho yake tulikaa kikao cha wanandugu na kuanza kumtafuta bila mafanikio ambapo mmoja wa marafiki zake waliokwenda wote kikazi Morogoro ndiye aliyetuambia alishuka Kimara na kusema anaenda kwa mpenzi wake.

Baada ya hapo, walikwenda kuripoti katika Kituo cha Polisi Kimara na kufunguliwa jalada la taarifa lenye namba KM/RB/2016 na kuambiwa waende kituo kikubwa cha polisi Gogoni ambapo mpenzi wa Denis alikamatwa kwa mahojiano na kueleza kuwa ni kweli alionana naye siku hiyo na walikaa pamoja kwa muda wa saa moja na nusu kisha baadaye, aliondoka na bodaboda.

 

Mpaka sasa mwanariadha huyo hajaonekana na kesi ipo Kituo Kikuu cha Polisi. “Naomba jeshi la polisi lifuatilie kwa kina suala hili maana sisi tupo njia panda hatujui hatma ya ndugu yetu kama amekufa au yupo hai maana ni bora tujue amekufa ili tuweke matanga,” alisema kaka wa Denis.

Toa comment