The House of Favourite Newspapers

Mwanasheria Dar Afungukia Hukumu ya DIAMOND, NANDY

Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’

DAR ES SALAAM: Kufuatia msala wa kusambaza video zao chafu mtandaoni unaowakabili mastaa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ na Faustina Charles ‘Nandy’, imeelezwa kuwa, endapo ikithibitika kuwa wamefanya kosa hilo, wanaweza kujikuta wakihukumiwa kifungo au kulipa faini ama kutumikia adhabu zote mbili.

 

Mwanasheria Emmanuel Elius wa jijini Dar, alipozungumza na Amani alisema sheria mpya ya mtandao, kifungu cha 14 kinaeleza kuwa iwapo mtu yeyote ambaye atathibitika na mahakama kuwa amesambaza picha chafu kwa njia ya kompyuta, simu au yoyote ya kielektroniki, atahukumiwa kutumikia kifungo cha miaka saba jela, kulipa faini ya shilingi milioni 20 au adhabu zote mbili.

 

“Hii ni kwa sababu sheria mpya ya mtandao iliyoanza kutumika mwaka juzi inatamka hivyo lakini adhabu hizo kama nilivyosema, ni baada ya kuthibitishwa na mahakama,” alisema mwanasheria huyo.

 

Faustina Charles ‘Nandy’

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, juzi aliliambia Bunge kuwa kuna baadhi ya wasanii ambao walianza kufanya uhuni ndani ya mitandao akiwemo mwanamuziki huyo nyota, Diamond Platnumz, ambaye tayari alikamatwa na polisi na kuhojiwa kutokana na picha alizosambaza mtandaoni.

 

Dk. Mwakyembe pia aliliagiza Jeshi la Polisi kumsaka msanii, Nandy ili naye ahojiwe kutokana na tuhuma kama hizo ambapo yeye video yake na Bill Nas ilisambaa mitandaoni wakijiachia kimahaba. Waziri Mwakyembe alisema hayo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM) aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani kutokana na wimbi la wasanii kuachia video za utupu mitandaoni.

 

Akifafanua zaidi Waziri Mwakyembe alisema Tanzania siyo kokoro la uchafu na kueleza kwamba wanaangalia taratibu za kuwafikisha Diamond na Nandy mahakamani kutokana na tuhuma hizo. Hata hivyo, Diamond alikamatwa Jumatatu (Aprili 16) na kuachiwa juzi Jumanne kwa dhamana ambapo ametakiwa kurudi Kituo Kikuu cha Polisi Cha Kanda Maalum kesho Ijumaa huku Nandy akiwa angali uraiani (tulipokwenda mitamboni juzi, Jumanne).

Stori: Mwandishi Wetu, Amani.

Comments are closed.