
Mwanaume mwenye umri wa miaka 47 nchini Vietnam amefariki dunia baada ya kuacha kutumia dawa zake za shinikizo la damu na badala yake kufuata ushauri alioupata kwenye mitandao ya kijamii. Ushauri huo ulimtaka anywe maji ya limao yenye chumvi nyingi na kuponya shinikizo la damu.
Kwa mujibu wa daktari Doan Du Manh wa Chama cha Magonjwa ya Mishipa ya Damu cha Vietnam, mgonjwa alifikishwa hospitalini tarehe 10 Desemba lakini alifariki kabla ya kupokelewa. Madaktari walibaini kuwa alipata mshtuko mkali wa ghafla wa shinikizo la damu (hypertensive crisis) uliosababisha kupasuka kwa mshipa wa damu kwenye ubongo.

Familia ilieleza kuwa alikuwa na historia ya shinikizo la damu kwa miaka kadhaa na alikuwa akifuata matibabu ya daktari. Hata hivyo, baada ya kujiunga na kundi la mitandaoni, alishawishika kuamini kuwa “dawa za kisasa zina madhara” na kwamba mwili unaweza “kujiponya wenyewe.” Licha ya kuombwa na mama yake asiache dawa, alisitisha matibabu na kuanza kunywa maji ya limao yenye chumvi nyingi na kuanika jua kwa siku 10 mfululizo ili ajitoe jasho.
Madaktari wanaeleza nini?
-
Shinikizo la damu ni ugonjwa wa kudumu unaohitaji matumizi ya dawa kwa muda mrefu ili kudhibiti hali.
-
Kuacha dawa ghafla husababisha “rebound hypertension” shinikizo la damu kupanda kwa kasi na kwa hatari.
-
Chumvi nyingi husababisha mwili kuhifadhi maji, moyo kufanya kazi kwa nguvu zaidi, na shinikizo la damu kuongezeka.
-
Kuani ka jua na upungufu wa maji mwilini huongeza mapigo ya moyo na mzigo kwa mfumo wa moyo na mishipa.
Mchanganyiko wa kuacha dawa, chumvi nyingi, na upungufu wa maji ulipelekea shinikizo la damu kupanda sana hadi kusababisha kupasuka kwa mshipa wa damu kwenye ubongo na kifo.
Onyo kwa umma
Wataalamu wa afya wanasisitiza:
-
Usiache dawa bila ushauri wa daktari, hata kama unajisikia vizuri.
-
Epuka “tiba” za kusikia-sikia, detox feki, na lishe kali zisizo na ushahidi wa kisayansi.
-
Dhibiti shinikizo la damu kwa vipimo vya mara kwa mara, dawa ulizoandikiwa, kupunguza chumvi, mtindo bora wa maisha na kudhibiti msongo wa mawazo.

