The House of Favourite Newspapers

MWANAUME ANAYEFAA KUKUOA ANATAKIWA AWE NA SIFA HIZI

HABARI za wiki hii mpenzi msomaji wa safu hii, ni matumaini yangu makubwa umzima wa afya na unaendelea vizuri na majukumu yako ya kimaisha bila wasiwasi wowote.

Mimi namshukuru Mungu kwa kuweza tena kunikutanisha nawe kupitia safu hii ambayo pamoja na mambo mengine nazungumzia mada mbalimbali zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.

 

Wiki hii nitazungumzia sifa za mwanaume ambaye anastahili kuutwa mume. Nafanya hivi ikiwa ni msaada kwa wale ambao wamefikia hatua ya kuingia kwenye ndoa lakini bado wanashindwa kutambua yupi ni sahihi na yupi si sahihi kuitwa mume.

Tufahamu kwamba si kila mwanaume unayekutana naye na ukampenda anafaa kuwa mumeo. Wengine wana mapungufu makubwa ambayo bila kuyabaini na ukaingia kichwakichwa, utakutana na matatizo makubwa.

 

Kwa maana hiyo basi, sifa ambazo nitazizungumzia leo endapo utaziona kwa huyo ambaye macho yako yameganda kwake, fanya maamuzi sahihi ya kumkubalia.

 

ANAKUPENDA KWA DHATI

Unapoingia kwenye maisha ya ndoa, unatarajia kupata mapenzi ya kweli kutoka kwa mwenza wako. Wapo wanaume ambao wanaonesha wazi kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa na mapenzi ya kuzuga.

Wanachotaka wao ni aidha kupata umaarufu tu kwamba yuko na demu flani bomba au kuonja tu penzi kisha kuanza visa ili muachane.

 

Kwa nini ni vizuri kumpata mwanaume mwenye mapenzi ya dhati? Hii inatokana na ukweli kwamba kinyume na hivyo, maisha yatakuwa ya migogoro kila siku. Atakufanyia mambo ya kukuumiza kwa kukusaliti bila kujali maumivu utakayopata. Hii yote ni kwa sababu hana mapenzi ya kweli na wewe.

Ndiyo maana unashauriwa kwamba, kabla hata ya kumuonjesha penzi kisha kufanya maamuzi ya kumruhusu aende kwa wazazi wako ili mfunge pingu za maisha, ni vyema ukawa na uthibitisho kwamba anakupenda kwa moyo mmoja.

 

TABIA ZAKE PIA

Linapokuja suala ndoa, tabia inakuwa kitu cha awali sana kuangaliwa. Hii ni kwa sababu, wapo wanaume ‘handsome’, wenye kazi nzuri na kipato kizuri lakini wanakosa sifa ya kuitwa mume kutokana na tabia zao chafu.

Hakuna mwanamke anayeweza kudiriki kumpa nafasi mwanaume kuwa mume wake wakati ana tabia chafu. Endapo utaangalia uzuri wa sura kisha ukafanya maamuzi ya kuolewa naye, utakuwa umejichimbia kaburi.

 

AWE ANAOTA MAFANIKIO

Hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko ya aina yake kwa wanawake. Wengi hawapendi kabisa kuolewa na mwanaume ambaye hana kazi.

Mwanaume anatakiwa kuwa dereva katika safari ya kusaka mafanikio, sasa kama atakuwa ni mtu wa kukaa kijiweni, kupiga mizinga, mvivu asiyependa kujishughulisha kwa namna yoyote, huyu hafai kupewa nafasi ya kuitwa mume.

Ile dhana ya kukubali kuolewa na mwanaume yoyote ili mradi upate heshima ya kwamba umeolewa, imepitwa na wakati. Mwanaume sahihi ni yule mwenye malengo maishani, anayefikiria nini cha kufanya kwa ajili ya maendeleo yake, mkewe na watoto wao.

 

WA SHIDA NA RAHA

Wapo wanaume ambao sio wavumilivu kabisa katika maisha. Tunajua maisha siku zote hayatabiriki, yanaweza kutokea matatizo ya kiafya ama kifedha.

Kwa mfano, unaweza kuingia kwenye maisha ya ndoa lakini kwa bahati mbaya ukawa huna kizazi, mwanaume mwenye mapenzi ya kweli na wewe anatakiwa kukuvumilia na kuwa upande wako.

Yule ambaye atakuwa anaungana na dada zake kukushambulia kwa kutozaa, hafai kuwa na wewe kwani yapo mengi yanayoweza kutokea yanayohitaji kuvumiliana.

 

Kimsingi uvumilivu kwa mwanaume utakuwepo kama tu atakuwa na mapenzi ya dhati kama nilivyozungumza hapo awali. Mwanaume mwenye mapenzi ya dhati ni lazima atakuwa mvumilivu na atakuwa tayari kuishi katika maisha ya aina yoyote, yawe ya raha ama ya starehe.

 

AIJUE THAMANI YA MKE

Wapo wanaume ambao hawajui thamani ya mume na ukiwachunguza utabaini hawafai kuwa waume za watu. Mume sahihi ni yule anayejua kwamba mke ni kitu cha faraja kwenye maisha yake.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.