The House of Favourite Newspapers

Mwandishi Salma Said apatikana Dar

0

Salma

Mwandishi wa Mwananchi na DW, Salma Said.

SIKU tatu baada ya mwandishi wa Mwananchi na DW, Salma Said kutoweka, jana alipatikana baada ya kukutwa katika Hospitali ya Regency ya jijini Dar es Salaam na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kuhojiwa.

Habari zilizopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mumewe, Ali Salim Khamis na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Simon Siro zilisema Salma alisajiliwa jana mchana katika hospitali hiyo.

Ali aliyekuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alisema kwa ufupi kuwa amepata taarifa hizo na kufika Dar es Salaam kuzifuatilia.

Kamanda Siro alisema ni kweli Salma amepatikana na ametumwa mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo kumfuata hospitali ampeleke kituoni kwa mahojiano.

Jana kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma kutoka Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti, ilisema inaendelea kufuatilia kwa makini kutoweka kwa Mwandishi wao wa Zanzibar, Bi Salma Said.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa, taarifa za kutoweka kwa Bi. Salma zilitufikia Ijumaa mchana tarehe 18 Machi 2016 kupitia kwa mume wake. Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote inayoonyesha ni nani au chombo gani kinamshikilia au kumhifadhi.

Hali hii inatutia wasiwasi mkubwa kama kampuni na wadau wa habari. Tunachukua fursa hii kuvitaka vyombo vya dola – vyenye dhamana ya ulinzi na usalama wa raia wake – kulitafutia ufumbuzi wa haraka suala hili ili kumaliza utata uliozingira kutoweka kwa Mwandishi Salma.
Ilisema taarifa hiyo.

Leave A Reply