The House of Favourite Newspapers

Mwanzilishi wa vyama vingi Tanzania-2

0

SAFU hii mpya ya Mleta Mabadiliko iliyoanza wiki iliyopita kwa kumuibua mwanzilishi wa vyama vingi nchini, James Mapalala inaendelea tena leo. Wiki iliyopita tulieleza jinsi mwanasiasa huyu alivyojitoa mhanga kupigania mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1968, miaka mitatu tu baada ya kufutwa na kujikuta akitiwa kizuizini na utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, Endelea:

Mapalala baada kupata misukosuko mingi alifanikiwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF) alichokiasisi mwaka 1991 kabla ya mfumo wa vyama vingi haujaingia rasmi nchini mwaka 1992.

Kiongozi huyu anakumbukwa na wengi kwa kupigania mfumo huo wa vyama vingi ambao umewafaidisha wengi wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani wa sasa ambao enzi hizo walikuwa serikalini.

Viongozi hao ni pamoja na Augustine Lyatonga Mrema, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye akiwa katika nafasi hiyo aliwahi kumfokea Mapalala kwa kumshawishi ili akubaliane na mfumo huo wa vyama vingi nchini.

Hivi sasa Mrema ni Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP) na amewahi kuwa Mbunge na Mjumbe wa Bunge la Katiba na walikutana na Mapalala ndani ya Bunge hilo wote sasa wakiwa wajumbe kutoka vyama vya upinzani.

Ndani ya Bunge hilo Mapalala pia alikutana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, chama ambacho Mapalala alikiasisi, kabla ya kufukuzwa, hao ni baadhi tu ya wanasiasa waliofaidika na juhudi za Mapalala.

James Mapalala alifukuzwa CUF kwa sababu zinazodaiwa kuwa za kidini mwaka 1994 akielekezewa pia tuhuma kama alizokumbananazo mwanasiasa kijana,  Zitto Zuberi Kabwe alipokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tuhuma za madai ya kutumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kuhusu hilo Mapalala  anafunguka: “Nilifukuzwa CUF kwa sababu za kidini tu. Ilikuwa mwaka 1994 baada ya kukijenga chama hicho nikashangaa mambo yamebadilika na viongozi wenzangu wamenigeuka. Wakawa wananishutumu kuwa natumiwa na CCM, mara nimechana bendera za chama na tuhuma nyingi tu. Lakini nilipata hadi nyaraka zilizothibitisha sababu za udini,” anasema na kuongeza:

“Lakini hata serikali pia ilichangia, nakumbuka siku ya mkutano wa kunifukuza kule Tanga, (mwandishi wa makala haya alikuwepo), Msajili wa Vyama vya Siasa (wakati huo), George Liundi (sasa ni marehemu) alikuwepo hadi saa tisa za usiku kuhakikisha kufukuzwa kwangu.”

Wanachama wa CUF walisahau kwamba Mapalala baada ya kuteuliwa kuwa mwenyekiti wao wa taifa mwaka 1993 alitembea mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar kukitangaza chama na alikuwa anakubalika kwelikweli.

Baada ya kufukuzwa Mapalala akaanza upya tena mikakati ya kuanzisha chama kingine. Hata hivyo, ilimchukua muda mrefu hadi Novemba 15, 2001 ambapo kwa fedha zake alifanikiwa kuanzisha Chama cha Haki na Ustawi (Chausta) alichonacho hadi sasa.

Tangu alipokianzisha alifanikiwa kupata diwani mmoja tu mkoani Mara mwaka 2005 ambaye hata hivyo hakuendelea baada ya kumaliza miaka yake mitano ya kuongoza.

Akizungumzia vyama vya upinzani vya sasa, Mapalala anasema kuwa vimejikita zaidi kwenye kutafuta madaraka badala ya kueleza sera zao kwa wananchi.

“Tofauti kati ya upinzani tuliokuwa tukiupigania miaka ile na wa sasa, ni watu kuwa na mawazo ya kwenda ikulu tu bila kusema watawafanyia nini wananchi baada ya kufika huko. Hata kwenye chama tawala, CCM, hali ni hiyo hiyo, watu wanalilia ikulu tu…,” anasema Mapalala.

Mwalimu Julius Nyerere katika hotuba yake ya kustaafu uenyekiti wa CCM mwaka 1990 aliungana na Mapalala bila kumtaja jina aliposema: “Lakini ni vizuri nikasema pia kwamba kwa maoni yangu hatuwezi tukaamua kuacha mfumo wa demokrasia ya chama kimoja, tukajaribu mfumo wa demokrasia ya vyama vyingi, kwa matumaini ya kwamba tukikuta kuwa mfumo huo hautufai, basi tutarudia tena demokrasia ya chama kimoja. Tutajidanganya, haiwezekani na ni vigumu kabisa.

“Demokrasia ya vyama vingi ikitushinda, mfumo ambao ni rahisi kufuatia utakuwa ni udikteta wa mtu mmoja au utawala wa kijeshi. Hiyo ni sababu nyingine muhimu ya kutofanya uamuzi kwa pupa!”

Lakini pia nina wasiwasi kwamba pengine sababu kubwa ya Mwalimu kuonesha kupendelea kurejea kwa mfumo wa vyama vingi ambao Mapalala alikuwa akiupigania tangu mwaka 1968 ni kwa kuwa yeye hakuwa tena rais wa nchi!

Niseme wazi kwamba Mapalala atakuwa kwenye historia ya uanzilishi wa vyama vingi katika nchi hii na wanamageuzi tunaowaona leo ni matunda yake.

MWISHO.

Leave A Reply