The House of Favourite Newspapers

Mwari we Unakimbilia Kwa Waganga, Nani Kakuroga?

0

Couple-in-BedMmh! Kweli tuna macho lakini  hatuoni, tuna masikio lakini hatusikii tukiitwa masanamu tutakasirika? Nasema tena kwa mdomo mpana baadhi yetu wanawake ni masanamu yenye damu. Hata ukinichukia ndiyo hivyohivyo, kama wewe ni mmoja wao unatakiwa kubadilika.

Ujinga wako wa kutotambua makusudi ya Mungu kukufanya mrembo, hakuwa na kusudio lingine kukurahisishia kuonekana kwa urahisi na kupata mume wa kukuoa. Uzuri wako unautumia vibaya mwisho wa siku mnafanya kila kona ya mji mabango ya waganga wa kienyeji yaongezeke kukudanganyeni eti kuna dawa za mapenzi na kukufanya uolewe.

Nakuuliza unakwenda kwa mganga ili uolewe nani kakuroga? Usinitumbulie mimacho kama dume la panya lililonaswa na mtego, nakuuliza wewe acha kuangalia pembeni.

 Ulipokuwa ukipendwa haukutaka kuolewa, wanaume wakija unaona wanataka kukuvunja kwani ule ndiyo wakati wako wa kuvunja mifupa ili uzeeni uwasimulie wajukuu zako.

Dada weee, wanaume nao hawapigiwi, hawajapigiwa wanacheza ukiwapigia unafikiri nini kitakachofanyika, utagombaniwa kama mpira wa kona na kujiona upo juu kumbe popo ukijisaidia unajichafua mwenyewe. Mwanaume akiwa na shida na kitu yupo radhi hata kuuza nyumba ya urithi ili tu akupate si unalipa wakati huo.

 Lakini uzuri haukai milele na mwili wa kuchezewa sana unapoteza mvuto na heshima mtaani, unajikuta ukiitwa majina ya kebehi Ooh, godoro la wanafunzi, mama huruma, jamvi la wageni au Call Box kila mwenye uwezo hujisevia.

Waswahili wanasema muda hausimami kila uvutapo pumzi hesabu dakika inakwenda, umri unasogea na uzuri nao unapotea. Pia haohao waswahili hawakukoma waliposema uanike wakati wa jua likiwa kali, lakini ukicheza nalo utautwanga mbichi.

 Walikuwa na maana nzito hasa kwetu wasichana, kuutumia usichana wetu vizuri hasa pale tunapopata nafasi ya kutaka kuolewa kutokana na Mungu kutujalia sura na maumbile.

Kuna dada mmoja ambaye wakati sisi ndiyo tunakua, alikuwa akitetemesha mtaa, kila mwanaume aliyemuona alitaka urafiki wenye fedha walishindana kutangaza ndoa. Badala ya kuchagua mwanaume mmoja amuoe atulie, yeye aliona fahari kubadili wanaume kama nguo kwa kuwa kishata mtaa. Mwanaume gani hakuujua mwili wake!

Baada ya kuugawa ovyo mwili wake kila mtu alimdharau, hakuna hata mwanaume aliyemfuata baada ya kujua maharage ya Mbeya, matokeo yake akawa mtu mwenye hadhi ya chini au uwanja wa mazoezi kwa wanaume wapenda ngono, hakuwa na tofauti na changudoa.

Aliokuwa akiwadharau waliolewa na kubakia mtaani peke yake kama genda eka ‘dume la nyani’. Naye akawa na hamu ya kuolewa lakini sifa yake mbaya hakuna mwanaume aliyejitokeza. Baada ya kujiona amedoda akawa kila siku kwa waganga kutafuta dawa ya mvuto, kweli wanaume aliwapata lakini hakukuwa na muoaji.

 Kila siku fedha yake iliishia kwa waganga, lakini sifa yake ndiyo iliyomkosesha wanaume kwa kuuchezea ujana wake, kuchezea maisha anaona jioni inaingia. Nani akuoe nawe kishata mtaa? Kwa tabia hizi tutazidi kujazana vibarazani kusubiri kuchukua waume wa wenzetu.

Jamani eeh, uzuri ni nafasi ya kuolewa, uutumie siyo kijidhalilisha na ukipoteza mvuto ukimbilie kwa waganga ili uolewe, Shuuutu unalo hilo.

Yangu yanatosha ujumbe umefika ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

Leave A Reply