Mwendawazimu Aliyefufuka-03

ILIPOISHIA…

Alipogeuka nyuma, akamwona jamaa anahangaia kuvuka barabara, wakati huo yeye tayari alikuwa amekwisha likabili daladala lililokuwa tayari kwa kuondoka. Upesi akatumia nafasi hiyo kuingia ndani ya daladala. Dereva akaliondoa gari.

Wakati anaketi kwenye kiti, mara jamaa mwenye kofia ya pama naye akawa amekwisha dandia basi hilo la Buguruni.

 

SASA ENDELEA…

KUTOKANA na utitiri wa abiria waliokuwa wamejazana ndani ya basi hilo, jamaa akajikuta ananing’inia mlangoni.

Mule ndani, Edna Manyanga alishuhudia kila kitu. Jamaa aliyekuwa anamfuata nyuma kama mkia alikuwa amepanda kwenye gari lile.

Mapigo ya moyo yalimwenda kasi, aliogopa sana, hakutaka kujidanganya kwamba mtu yule akipata nafasi pweke hawezi kumfanya kitu mbaya. Kitendo cha kumwona akilipanda gari alilopanda yeye alitishika.

 

Wakati basi hilo likiwa kwenye foleni, katika mataa ya Gerezani, Kariakoo, ikingojewa taa ya kijani iwake ili gari hilo liwe na sheria ya kuvuka kwenye makutano ya barabara. Edna akili yake ilikuwa ikimzunguka kwa kasi ya kompyuta.

Kule kwenye mlango wa kondakta watu walikuwa wamebanana kiasi kwamba kama kuna mtu angehitaji kuteremeka, ingewalazimu watu wote waliokuwa wamesimama eneo lile la mlango, wateremke kupisha njia.

 

Edna akiwa amejituliza kwenye kiti cha dirishani, kwa jicho la chinichini, aliuona mkia wake. Alikuwa ni moja ya watu waliorundikwa na kondakta kwenye mlango wa gari hilo kama ndizi.

Alipoyarudisha macho yake nje. Mawazo fulani yakawa yanajitengeneza akilini mwake, akawa anawaza.

Apitie dirishani, aruke kisha atimue mbio. Akaamini bila shaka atakuwa amempoteza kabisa ule mkia uliojituliza kwenye mlango wa kondakta, unaomfuata kama kivuli.

 

Lakini wazo jingine likamjia, akafikiri hatakiwi kufanya hivyo, kitendo cha kuruka kupitia katika dirisha la daladala, kivyovyote angeonekana mwizi au mwendawazimu. Hakutaka kujiongopea kwamba isingezua kizaazaa.

“Nifanyeje sasa Mungu wangu, nitashikwa mimi!” alinong’ona.

Uso wake ulisawijika kwa mashaka na wasiwasi. Gari liliendelea kusimama kungoja taa ya kijani na kadiri muda ulivyozidi kusogea ndivyo msukumo wa fikra za kutorokea dirishani zilivyozidi kutekenya utashi wake.

 

Dar es salam, watu wanagombea usafiri wa daladala kila kuchwao. Wengine hupitia madirishani ili wapate kiti. hata hivyo, abiria hawapigani vikumbo wakati wa kuteremka. Sasa iweje arukie dirishani, tena kwenye mataa. Alisikia sauti mojo akilini ikimtahadharisha.

“Sasa nifanye nini?”

Hili swali halikuwa na jibu.

Katika kuangalia angalia nje, kulia na kushoto. Kwa bahati, akamwona machingammoja anauza ushungi. Kuona bidhaa hiyo akili yake ikafanya kazi haraka sana.

Akamwita yule muuzaji.

“Shilingi ngapi?” aliuliza huku akifungua pochi yake na kutoa noti ya elfu tano.

“Elfu mbili tu.”

 

“Nipe huo mweusi.”alisema huku akimpa ile noti ya elfu tano.

Upesi machinga akampa ule ushungi na kabla hajarudisha chenji taa ya kijani ikawaka!

“Chenjiiii!!” muuzaji alipiga kelele na kulikimbuilia gari.

“Utakunywa soda.” Edna alimjibu.

 

Gari likavuka mataa ya gerezani, likanyooka na njia kuelekea Ilala boma. Pale kitini, Edna alijitanda vizuri ushungi ule. Akafungua mkoba wake na kuchagua miwani moja kati ya mbili zilizokuwemo. Akatoa ile nyeusi maalumu kwa jua. Baada ya kuivaa angalau mwonekano wake ukabadilika.

Dakika chache badaye, gari lilikuwa linakaribia mata ya Ilala boma. Bahati nzuri askari aliyekuwa amesimama kwenye njia panda zile, alikuwa akiita magari ya upande wao.

Daladala lile la mjini lilivuka eneo lile la njia panda. Dakika zingine chache kondakta akawa anawatangazia watu wanaoshukia kituo cha Amana.

 

Edna mtoto wa mjini, alitambua kituo cha Amana abiria wengi wanateremka pale, akaona naye anaweza kutumia fursa hiyo kushuka kituo kile kile. Na akaamini kwa mwonekano mpya aliokuwa nao labda angeweza kumkimbia jamaa aliyekuwa anamwinda.

Gari liliposimama, watu wengi wakawa wanateremka. Wale abiria waliokuwa wamelundikana pale mlangoni kwa kondakta waliteremka chini wote.

 

Kuna baadhi yao nao walikuwa wamefika. Walimlipa konda na kuondoka. Wengine walikuwa bado wanaendelea na safari. Walibakia walisimama kando kusubiri washukaji waishe kisha warudi garini kuendelea na safari.

Mkia’ uliokuwa unamfatilia Edna ulikuwa miongoni mwa abiria walionekana kuendelea na safari. Alisimama kando.

Edna akiwa makini na jamaa huyo, uso wake ukiwa chini. Baada ya kuteremeka garini, alimpa konda pesa yake. Kisha akazipiga hatua za kunyata akiliacha gari hilo.

 

Alipotizama kwa hila, akamwona jamaa bado amesimama kando ya mlango wa daladala, akingoja abiria wanaoteremka ili arudi garini.

“Hajanigundua, hajaniona!!” alinong’ona. Uso wake ukajaa shauku ya kutoweka kabisa eneo lile kabla jamaa hajagundua kwamba ameachwa.

Alimwita derava Bodaboda na kumuamuru ampeleke Sinza.

“Hadi Sinza ni elfu kumi ant…”

 

“Endesha pikipiki acha upumbavu.” Edna Manyanga alifoka. Hakupenda kupoteza muda.

Dereva bodaboda, akaindoa kwa kasi pikipiki ile aina ya boxer. Naye ile elfu kumi aliitaka sana.

Wakati Edna Manyanga na dereva bodaboda wanatokomea eneo lile la Amana, kule kwenye daladala, baada ya nusu ya abiria kuteremka, wale watu waliokuwa kando ya mlango, wakarudi garini kuendelea na safari iliyokuwa imesalia.

Moyo wa Merick Stephano, ulipiga kite baada ya kutoliona windo lake kwenye kiti alipokuwa ameketi.

“Yuko wapi?” alinong’ona. Wakati huo basi lilikuwa limekwisha changanya moto.

 

Kutomwona mwanamke huyo kukamfanya akili yake ipagawe.

“Nishusheee!!!” alibweka kwa sauti kali. Dereva akalisogeza gari pembeni huku akitokwa na maneno ya lawama. Merick akateremka garini bila kujali lawama za dereva na kondakta wake.

“Huyu mwanamke ameniachaje!?” alinong’ona tena peke yake.

Aliamini kivyovyote mwanamke huyo alimtoroka wakati abiria wakiwa wanateremka pale Amana, lakini alipita pitaje mlangoni pasina kumwona… Aliendelea kujiuliza akilini. Na inamaana amekwisha nigundua kwamba namfutilia?

 

Kazi yake hiyo aliyopewa na wakubwa wake aliyoiona ni rahisi sana, hasa kwa kuwa mtu mwewenye alikuwa ni mwanamke. Lakini sasa ilianza kuwa na viashiria vya ugumu.

Itaendelea wiki ijayo…

kitabu cha ‘DAMU YA MWANAMWALI’ kipo mtaani. Bei yake ni elfu kumi(10,000/=).

 

ALLY KATALAMBULA | +255 687 750295

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club


Loading...

Toa comment