MWENDAWAZIMU ALIYEFUFUKA – SEHEMU YA 2

ALIPOISHIA…

“She was attaked!!!!..” alibweka tena kwa fadhaa akishuhudia yule mrembo akigaa gaa chini kwa maumivu huku damu ikimchuruzika.

Akaona kuendelea kupoteza sekunde za kumwangalia binti yule ni kupoteza muda dhidi ya adui. Akarudisha umakini kwenye bunduki yake. Hata hivyo alikwisha chelewa. Alichelewa muda mrefu sana!!!!!!!

 

ENDELEA NAYO…

RISASI moja ilichimba pembeni kidogo ya bega lake la kulia. Alipiga yowe moja la uchungu halafu akapiga kimya cha ghafla, akabakia akiugulia ndani kwa ndani. Maumivu makali yakasambaa mwili mzima. Almanusra aanguke chini ya mti huo, kwa bahati alibaki amelikumbatia tawi la mti.

Ile bunduki yake ya masafa marefu nayo ilibaki ikining’inia chini. Ilikuwa ni kama bahati tu kwa ni mkanda wa bunduki hiyo uliuvaa kifuani.

 

Alibaki amejikunyata pale tawini, ametulia tuli. Kwa sekunde hapakuwa na mashambulizi yeyote, hakuna kilichosikika zaidi ya yowe la mwanamke chini ya mti sambamba na matone ya mvua.

Giza lilikuwa ni zito ndani ya msitu huo wa Goma. Kama hutumii darubini zenye uwezo mkubwa, basi kwa macho ya kawaida kamwe yasingeweza kuona japo umbali wa sentimita 120.

Mara chache miale ya radi ilipowaka, ndipo nuru ya mwanga iliangaza sehemu kubwa ya msitu, ungeweza kuona namna matawi ya miti na majani yanavyosukwa sukwa na upepo uliokuwa unavuma kwa nguvu.

 

Mpiganaji yule aliyekuwa amebana kwenye tawi la mti ule mkubwa, akiwa tayari amekwisha jeruhiwa, kupitia uzoefu wake kwenye medali za kivita, aling’amua adui anayemshambulia ni ‘sniper’ yaani mdunguaji ambaye anashambulia kwa hesabu kali.

Hakujua adui huyo anatokea upande upi. Alijiuliza: Je, ni kile kichaka alichokiona kupitia darubini ya kwenye bunduki yake kikiwa kinanyata?

 

Lakini hapana! Mtu yule aliyejivika majani na magome ya mti kiasi cha kumtengenezea taswira kama ya kichaka, alikuwa mbali na mazingira ya eneo alilokuwepo, kamwe isingekuwa rahisi kuonekana.

Swali kuu likaendelea kubaki kuwa, adui anayemshambulia yuko wapi? Na vipi mwanamke anayebweka kwa maumivu hapo chini ya mti?

Mwanamke ambaye usiku huo ingembidi awe anahudumia mumewe haki yake ya ndoa. Anafanya nini ndani ya uwanja wa vita. Ni nani huyu mwanamke na kwa nini anashambuliwa? Je, adui yetu ni mmoja? Yeye amewakosea nini maadui zetu?

 

Jamaa alijiuliza. Akili yake ilimzunguka kwa kasi sana, alimini ipo sababu inayojibu kwa nini binti yule anashambuliwa na maadui zake. Hakujua na hakuona njia ya kupata majibu ya maswali hayo zaidi ya kuikoa roho yake.

Aliamini kama akizubaa, uwezekano wa kufa kizembe ni mkubwa. Wakati huohuo, yule mwanamke kule chini aliendelea kupiga kelele za maumivu makali. Ajabu mdunguaji hakummalizia.

“Hii ina maana gani?” alinong’ona. Alihisi uwepo wa mtego. Alikuwa makini sana. Kosa moja lingempeleka akhera.

 

Akiwa amekumbatia tawi lile la mti, maumivu yakiendelea kutambaa kwa kasi mwilini mwake. Mwanaume akajikaza kisabuni, akawa anaivuta bunduki yake iliyokuwa inaning’inia.

Lilikuwa ni kosa kubwa.

“PaAAA!.. PaaAAA..! KbbBUUM!!… Chwaaarr!!!”

“Yalaa!!”

 

Mlio wa vyuma vikigonga ile bunduki na vingine vikiparaza gome la mti vilisikika! Mpiganaji yule kwa mara nyingine, alipiga yowe la uchungu. Risasi nyingine ilikuwa imembamiza mkononi mwake.

Na katika hali asiyo iratajia bunduki yake ilianguka chini kabisa ya mti ule.

Alikuwa amejeruhiwa vibaya sana. Risasi ilikuwa imechimba kwenye kiganja cha mkono wake na kutoboa tundu baya lililo tiririsha damu kama bomba la maji lililofunguliwa koki.

“Blood Coward, nakufa, sina ujanja” Jamaa alibweka. Na kweli alikuwa hana ujanja. Siku hiyo ilikuwa ni Arobaini yake. Adui alikuwa amemdhibiti karibu kona zote. Kifo chake kilikuwa sentimita chache mbele yake.

**

 

KARIAKOO – TANZANIA

Edna Manyanga, mwandishi wa habari wa kujitegemea. Alizipiga hatua za harakaharaka huku moyoni akiwa na hofu na mashaka makubwa. Alitembea akiupita mtaa wa Gerezani, akavuka barabara na kukifuata Kituo cha Daladala cha Agrey.

Alikuwa anatembea huku akiwa ameshikilia mkoba wake kwa makini sana. Umakini na mkoba huo sio dhidi ya vibaka waliotapakaa kila kona mjini Kariakoo. Laa! Bali thamani ya vitu vilivyokuwa ndani ya mzigo huo.

 

Ndani ya mkoba kulikuwa na kamera, kamera ya siri mfano wa miwani ya macho, ambayo alikuwa akiitumia kwenye kazi zake mbalimbali za kichunguzi.

Siku hiyo, ndani ya memori kadi ya kamera hiyo ilikuwa imebeba jambo zito tena la kutisha na kwa kweli kama jambo hilo mwandishi huyo ataliweka hadharani basi nchi ingesimama kwa muda. Ilikuwa ni siri ya kuogopesha sana.

Mwandishi huyo aliyebobea kwenye habari za kichunguzi, alikuwa na miaka takribani saba kwenye taaluma hiyo. Pamoja na umahiri wake wa kuibua habari mbalimbali za kichunguzi, hakuwahi kupata habari kubwa na ya kusisimumua kama ambayo alikuwa amepata siku hiyo.

 

Alikuwa ametembea kwa mguu akitokea mtaa wa Lindi, ambako alishuka kwenye bodaboda ambayo aliikodi akitokea Oysterbay, ambako huko ndiko alikopata tukio lililokuwa ndani ya mkoba wake.

Ilikuwa ni habari iliyobeba skendo chafu ya kiongozi mkubwa wa nchi. Tena ambaye yupo katika idara nyeti ya usalama wa nchi.

Edna Manyanga, alikuwa na hofu, alitembea kuliendea gari lililokuwa likipakia abiria. Tangu aliposhuka kwenye bodaboda kule mtaa wa Lindi, nyuma yake kulikuwa na mwanaume aliyekuwa amevalia kofia ya pama, ambaye alikuwa akimfuata kwa karibu sana.

 

Mtu huyo ndiye alikuwa akimtia wasiwasi. Hakujua alianza kumfutilia kuanzia wapi, Edna Manyanga alibaini kufuatiliwa muda mchache baada ya kushuka kwenye bodaboda ni baada ya yeye mwenyewe kufutulia nyendo za watu waliokuwa nyuma yake. Ndipo mtu mwenye kofia ya pama alipogundulika.

Alipogeuka nyuma, akamwona jamaa anahangaika kuvuka barabara, wakati huo yeye tayari alikuwa amekwisha likabili daladala lililokuwa tayari kwa kuondoka. Upesi akatumia nafasi hiyo kuingia ndani ya daladala. Dereva akaliondoa gari.

Wakati anaketi kwenye kiti, mara jamaa mwenye kofia ya pama naye akawa amekwisha da ndia basi hilo la Buguruni.

Itaendelea wiki ijayo.

ALLY KATALAMBULA | +255 687 750295

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club


Loading...

Toa comment