The House of Favourite Newspapers

Mwenzi Wako Akikuonyesha Haya, Jua Hakutaki!

Related image

KWA kawaida mtu anapompenda mtu huwa ni vigumu sana kumuacha aende. Hatamani hata siku moja kumpoteza mtu ampendaye. Atafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba mhusika anakuwa mpenzi wake.

Mapenzi humfanya mtu awe kipofu. Anashindwa kufikiri sawasawa na kufanya maamuzi sahihi. Hisia kali za mapenzi zinampeleka ndivyo sivyo yeye anaamini yupo sahihi.

Mtu wa namna hii, mara nyingi ambaye hayajamkuta huwa anaweza kumuona kama vile ni punguwani au mshamba wa mapenzi lakini kumbe hata huyo anayemcheka mwenzake, naye yanaweza kumkuta mambo ya aina hiyohiyo. Ni vigumu sana kutambua kama hayajakukuta. Mtu wa nje anaweza kukupa majina ya kila aina lakini kimsingi wakati ule unakuwa si wewe bali ni ‘kutekwa penzini’.

Ndio maana leo nimekuja na mada hii kwa ajili ya kukukumbusha kwamba kuna mambo ukiyaona kwa mwenzi wako basi ujue kabisa mhusika hakupendi bali anakufanya wewe kama mtu wa ziada. Anakufanya wewe kama changuo la pili, uwepo au usiwepo kwake ni sawa tu maana haupo tena  moyoni mwake.

HANA HABARI NA WEWE

Ukiona mwenzi wako hana muda na wewe, haulizi umeamkaje wala unaendeleaje kwa siku ya kwanza na hata ya pili basi unapaswa kujua kuna tatizo.

Ukifanya uchunguzi kwa kujitathimini kuwa mara nyingi wewe ndio unayemjulia hali, yeye hafanyi na ukiacha basi ndio imetoka basi ujue tu hapo hupendwi.

Mfanyie uchunguzi wa muda mrefu mtu wa aina hiyo na ukiona tatizo hilo linazidi kuendelea basi anza kukaa naye mbali. Jaribu kukaa kimya na ukiona amekaa hata zaidi ya mwezi mmoja hakuulizi hata uko wapi, unarudi nyumbani saa ngapi na mambo mengine kama hayo basi ujue hakupendi.

HAKUPIGII SIMU

Ukiona mtu wako yeye hana muda wa kukupigia simu hadi wewe umpigie, ukiaacha anaweza kukaa hata mwezi mzima na ukimfanyia tathimini unaona kabisa si mtu wa kukosa vocha muda wote huo basi jua kabisa ana lake jambo.

HAHITAJI MUONANE

Ukiona mwenzi wako kila wakati anajifanya yuko bize, mkiweka miadi ya kukutana kila siku hakosi visingizio basi unapaswa kuanza kujiongeza. Usipaniki bali mweke kwenye mtego wa muda fulani, muangalie sarakasi zake za kukuchenga zitakwenda hadi lini.

Unapoona sarakasi hizo zinakuwa nyingi, usihangaike naye. Kaa kimya kwa muda fulani na mwisho wa siku utakuja kubaini kwamba hakuhitaji, kama akikutafuta kwa kujistukia mpe muda pia wa kuona kama kweli anahitaji kuwa na wewe au kukupotezea muda. Wengi wanaopanga kucheza na mtu huwa hawawezi kudumu muda mrefu, atajisahau tu tena na kurudi kwenye sarakasi zake alizozizoea.Image result for black african couples ARGUE

HATAKI UJUE  RATIBA ZAKE

Ukiona mtu anakukwepa, hataki ujue ratiba yake, hataki uwajue watu wake wa karibu na mpo naye kwenye  uhusiano kwa muda mrefu kidogo basi ujue kabisa hana dhamira njema na wewe. Macho yake bado yanahangaika kutafuta na akipata kwingine atakuacha!

KUFOKA BILA SABABU

Ukiona mwenzi wako anafoka hovyo, jambo dogo anakuja juu na ukizingatia hakuwa hivyo wakati mnaanza uhusiano basi ujue fika anakutafutia sababu.

Jambo dogo kwake linakuwa kubwa, atakasirika siku mbili hadi tatu hamuongei. Hata ikitokea mmeongea, baada ya muda tena anakucharukia bila sababu ya msingi. Ukiona mtu wa aina hiyo na bado hamjafika mbali kwenye uhusiano basi ni bora ukaanza kumuepuka na kusubiri upate mwenza sahihi wa maisha yako. Tukutane wiki ijayo.

Comments are closed.