Mwili Wa Mwanamuziki Tabia Mwanjelwa Kuzikwa Leo Mbeya
Mwili wa mwanamuziki mkongwe, Tabia Shabani Mwanjelwa, aliyefariki Januari 25, 2025, huko Saarbrücken, Ujerumani, umewasili Dar es Salaam jana na unatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Kiwira, wilayani Rungwe, Mbeya.
Binti wa marehemu, Jane Jackson, alisema mwili wa mama yake uliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ndege ya Ethiopian Airlines, ukiambatana na mume wa marehemu, Bw. Elmar Moessner, na mtoto wake wa kiume, Moses.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo, alikuwepo kuongoza mapokezi ya mwili huo.
Hata hivyo, wanamuziki na wadau wa muziki na hata wanahabari hawakujitokeza kwa wingi kama ilivyotarajiwa, hali iliyozua maswali mengi.
Marehemu atakumbukwa kwa vibao maarufu kama “Jane Mimi Nahangaika” na “Kweli Maisha ni Safari Ndefu”, alizoimba na Maquis Du Zaire miaka ya 1980.
Licha ya kuishi Ujerumani kwa zaidi ya miaka 40, alikuwa akirejea Tanzania mara kwa mara kusalimia ndugu na jamaa.
Kwa mujibu wa Jane, mama yake alisumbuliwa na uvimbe kooni kwa muda mrefu, na wosia wake ulikuwa azikwe Kiwira alikozaliwa.
Jane, ambaye ndiye aliyeimbwa na mama yake katika kibao cha “Jane Mimi Nahangaika” amesema kwamba mazishi yanatarajiwa kufanyika leo saa saba mchana Kiwira Mbeya.
Mungu ailaze pema roho ya marehemu.
Na Elvan Stambuli, GPL