Mwili wafukuliwa, wavuliwa sare za kazi

 

SERIKALI magharibi mwa Kenya imefukua mwili wa mkazi mmoja ili kumvua sare alizozikwa nazo kulingana na ripoti.

Martin Shikuku Alukoye alizikwa akiwa na sare zake za huduma ya vijana wa Kaunti ya Kakamega baada ya kufa maji mwezi huu ambapo baadaye maofisa wa kaunti hiyo waliufukua mwili wake ili kumvua nguo hizo kulingana na ripoti. Hata hivyo, mjomba wa  marehemu huyo alisema kwamba waliofanya hivyo walikiuka sheria za nchi na utamaduni husika.

”Tuliishirikisha kamili serikali ya kaunti katika mipango ya mazishi na hawakupinga pendekezo letu la kumzika akiwa na sare za kazini,” alisema Francis Mutamba kulingana na gazeti la Daily Nation.

Familia hiyo inasema kwamba ilipinga ombi la maofisa hao kuchukua nguo hizo baada ya  kuzikwa kwa jamaa huyo mwenye umri wa miaka 31, na kwamba maofisa hao  waliamua kuufukua mwili huo bila idhini yao au agizo la mahakama.

Wakati huohuo, naibu chifu wa eneo la Ituti, Daniel Namayi alishutumu ufukuzi huo na kuonya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya maofisa husika.

”Mara tu mwili unapozikwa, huwa panahitaji agizo la mahakama kwa mtu yeyote mwenye malalamiko ya kutaka kuufukua. Wasimamizi wa kaunti wameenda kinyume na sheria kwa kuufukua mwili huo, suala ambalo ni kinyume na utamaduni.

”Tuliamua kumzika mwana wetu usiku kuambatana na tamaduni ambazo zinasema kwamba mtu aliyekufa maji hapaswi kuzikwa wakati kuna mwanga wa jua . Lakini maofisa wa kaunti wametushangaza wakati walipoamua kuufukua mwili ili kuchukua sare alizozikwa nazo, ” alisema Mutamba.

Pamoja na hayo, mwili huo ulivishwa nguo mpya na kuzikwa tena mapema wiki hii baada ya wazee kufanya matambiko ya kuitakasa familia hiyo.

Chanzo: BBC SWAHILI


Loading...

Toa comment