The House of Favourite Newspapers

Mwinjilisti Silvanus Ngemera Afunguka Ujio Wa Dini Ya Kiafrika

0

MWINJILISTI Silvanus  Ngemera amekuja na ujio mpya wa dhehebu linalojulikana kwa jina la African Orthodox Derekh ambapo kupitia dhehebu hilo amedhamiria kuuondoa ukristo wa kikoloni na kuifundisha jamii ukiristo wa Kiafrika ndani ya nchi 42 za Kiafrika Kusini mwa Sahara.

Hayo ameyasema Septemba 6, 2024 katika ukumbi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere jiji Dar es Salaam.

Mwinjilisti Ngemera amesema kuwa Derekh  ndilo jina lililotumiwa na Kanisa la kwanza pale Yerusalemu lenye maana ya NJIA YA MUNGU.

“UKRISTO WA KIAFRIKA ni ule ulioshikamana na Utamaduni chanya wa Mwafrika bila kujumuisha Miungu, Mizimu, Uaguzi, kuloga, Uchawi, Matambiko, Ramli na Dhambi zingine,” amesema Mwinjilisti Ngemera.

Aidha Ngemera alieleza sababu ya kuunda dhehebu la Waafrika, kuwa, Madhehebu yote ya Ukristo Afrika Kusini mwa Sahara ni matawi ya Madhehebu ya Ulaya na Marekani, na kwa jinsi hiyo yanaongozwa Kutoka Ulaya na Marekani.

Amesisitiza kuwa kuunda dhehebu moja kwa Waafrika wote kutoka Cape Town, Juba, hadi Accra na kuyakataa Madhehebu ya kigeni na makanisa binafsi ni suala la msingi ili kuwa na umoja wa Ukristo wa Waafrika kwa kuwa wa Wazungu hauna maslahi kwa Waafrika ki-imani na ki-wokovu.

Mwinjilisti huyo ameendelea kueleza kuwa AFRICAN ORTHODOX DEREKH ni taasisi kubwa ya Mungu, isiyomilikiwa na mtu yeyote bali inamilikiwa na Mungu na kuongozwa na Mchungaji Yesu na Waamini wote.

“Tukisha kufanya uamuzi huu wa kujitenga kiuendeshaji na Ukristo wa Wazungu na kuchukua upya Ukristo Kutoka kwenye shina lake mjini Yerusalemu kama tunavyoruhusiwa na Bibilia yenyewe, basi tunalazimika pia kuunda upya Teolojia, Katekizimu na Liturujia yetu,” ameongenza Mwinjilisti Ngemera,

“Tunalazimika pia kuondoa uchakachuaji wa dini uliofanywa na madhehebu ya kale kwa kujitungia baadhi ya mambo, kuyanyamazia mambo yaliyo muhimu kwa dini hii, na kuingiza mambo ambayo hayamo kwenye Biblia au hata yanayopingana nayo,”.

Hivyo Ngemera amefafanua kuwa, dhehebu hilo ni la Mungu, na litamlenga Mungu zaidi katika mafundisho yake ambapo ameeleza kuwa Mungu ni mmoja na wanaikataa hoja potofu ya utatu mtakatifu

Leave A Reply