The House of Favourite Newspapers

Mwisho wao leo

0

DONALD-NGOMA2.jpgHAKUNA sentesi nyingine zaidi ya ‘Mwisho wao leo’, kwani Yanga na Azam FC zinapambana leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Ligi Kuu Bara.

Timu zote mbili zinaingia uwanjani na kumbukumbu zisizo sawa kuhusu mechi zao za mwisho, ndiyo wote wamepania kumaliza ubishi kwenye uwanja huo jioni kuanzia saa 10:00 huku mwamuzi huyo akiwa Kennedy Mapunda.

Katika mechi za ligi kuu kuanzia msimu wa 2011/12 hadi leo, timu hizi zimekutana mara tisa na Azam imeshinda mechi nne, Yanga imeshinda mara mbili lakini zimetoka sare tatu.

Kwenye mechi hizo, Azam imefunga mabao 13 na kufungwa 11 wakati Yanga imefunga 11 na kufungwa 13.

Stewart-HallKocha wa Azam, Stewart Hall

Kocha wa Azam, Stewart Hall ameacha majukumu ya kuzungumzia mchezo huu kwa msaidizi wake, Mario Marinica, ambaye amenukuliwa akisema hawana hofu na Yanga kwani wamejiandaa vya kutosha.

“Tumecheza na Yanga mara nne msimu huu kwenye michuano tofauti, hawajaweza kutufunga mchezo hata mmoja, uliona kilichotokea kwenye mchezo wetu wa mwisho na Yanga? Walizawadiwa penalti ambayo haikuwa halali,” alisema Marinica raia wa Romania.

Kwa upande wake, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm alisema: “Mechi na Azam ni mchezo mgumu sana, lakini kambi yangu imenipa matumaini na nina uhakika tutashinda na kusonga mbele. Lengo letu ni kubaki kileleni tu.”

Mara ya mwisho Yanga na Azam kukutana ilikuwa ni Januari, mwaka huu katika Kombe la Mapinduzi mjini Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan ambapo zilitoka sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo, nahodha wa Azam, John Bocco alitolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi.

Yanga ipo kileleni mwa ligi kuu ikiwa na pointi 46 sawa na Azam iliyo nafasi ya pili lakini tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga ndiyo inayowaweka Wanajangwani kileleni.

Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45, hivyo sare katika mchezo wa leo itatoa nafasi kwa Wekundu wa Msimbazi kileleni endapo kesho watashinda dhidi ya Mbeya City katika ligi hiyo.

Vita zaidi katika mchezo wa leo itakuwa kati ya;

Ngoma na Wawa

Beki Pascal Wawa atakuwa katika nafasi nyingine ya kupambana na Donald Ngoma katika mchezo huu, mara kadhaa wanapokutana wawili hawa shughuli huwa pevu. Ngoma amewahi kuifunga bao moja Azam.

 

Tambwe na Morad

Vita nyingine ni kati ya Amissi Tambwe wa Yanga na Said Morad wa Azam, mara zote wanapokutana huwa na purukushani kubwa wanapowania mpira. Morad anasifika kwa kutumia nguvu wakati Tambwe ni ujanja na ‘timing’ tu.

Himid na Kamusoko

Kiungo wa Azam, Himid Mao na Thabani Kamusoko wote wapo kwenye ubora wao, hivyo kutakuwa na vita kubwa kati yao leo kama wakipata nafasi ya kuanza.

 

Niyonzima na Mugiraneza

Nyota wa zamani wa APR, Haruna Niyonzima wa Yanga na Jean Piere Mugiraneza ‘Migi’ wanaweza kukumbuka wakati wakiwa APR, watapambana katika timu mbili tofauti, mmoja akizubaa mwingine ataonekana si lolote.

Yondani na Bocco

Raha nyingine ipo kuwatazama Kelvin Yondani wa Yanga anapopambana na straika wa Azam, Bocco. Kwenye mechi ya Kombe la Mapinduzi, Bocco alitolewa nje kwa kadi nyekundu iliyosababishwa na Yondani baada ya kutupiana maneno na kurudishiana rafu.

Pluijm na Stewart

Makocha wazungu, Pluijm raia wa Uholanzia wa Yanga na Hall raia wa Uingereza wa Azam, wote wana nafasi ya kuthibitisha ubora wao kwani wanawania ubingwa lakini mwisho mashabiki watataka kuona nani ni zaidi katika kupanga kikosi.

Pluijm amekuwa mpenzi wa kutumia mfumo wa 4-4-2 au 4-5-1, huku Hall yeye akipenda zaidi kutumia 3-5-2. Kazi ipo ila mwisho wao leo!

Said Ally, Dar na Suleiman Hassan, Pemba

Leave A Reply