Mwongozo wa Kusimamia Miradi ya Kimkakati Kusaidia Kuongeza Mapato Katika Halmashauri

ILI kukabiliana na changamoto za usimamizi duni wa miradi, ukosefu wa utaalamu wa kutosha miongoni mwa watumishi, kuchelewa kukamilika kwa miradi na mingi ya miradi hiyo kutotekelezwa kwa viwango vilivyotarajiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, serikali imezindua mwongozo wa uanzishwaji na usimamizi wa kampuni mahsusi za uendeshaji wa miradi ya vitega uchumi kwenye serikali za mitaa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dodoma leo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Adolf Ndunguru alisema mwongozo huo ni zana mpya ya marejeleo kwa timu za halmashauri utakaotoa mwongozo, hatua kwa hatua wa jinsi ya kuanzisha na kusimamia miradi ya kimkakati ya kuzalisha mapato kwa kutumia makampuni (SPV).
“Mwongozo huu ni suluhisho la changamoto nyingi zinazozikabili halmashauri zetu katika kusimamia miradi ya vitega uchumi katika eneo la utawala, uendeshaji na usimamizi wa fedha.

“Mwongozo huu unaotoa fursa ya mawazo mapya na njia za kibunifu za kuimarisha makusanyo ya fedha, kuimarisha uwezo wa kiufundi wa kusimamia uwekezaji wao wa kimkakati wa kuzalisha mapato na hatimaye kuongeza mapato ya ndani na kuboresha utoaji wa huduma katika ngazi za mitaa, unapaswa kutumiwa na mamlaka zote za serikali za mitaa, ikiwemo bodi za kampuni za kusimamia miradi (SPVs)”, alisema Ndunguru.Pamoja na hayo, alisema tangu mwaka wa fedha wa 2017/18, serikali imefanikiwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 294.96 kwenye miradi 46 ya kimkakati, ambapo miradi 26 ikiwa imekamilika.

“Serikali inatoa shukurani zake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kwa ushirikiano wao endelevu, msaada wa kitaalamu na kifedha katika kuandaa mwongozo huu pamoja na mafunzo ya kuwajengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) juu ya matumizi ya mwongozo huu,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Shirika la UNCDF, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Johnson Nyella, ambaye pia ni Kamishna wa Sera wizarani hapo alisema serikali imekuwa ikigharamia ujenzi na utekelezaji wa miundombinu ya uwekezaji ya kuongeza mapato kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha ikiwemo za miradi ya kimkakati.
“Ni matumaini ya serikali mwongozo huu utaimarisha uwezo wa kitaalamu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika usimamizi wa miradi ya uwekezaji ya kuongeza mapato, hivyo kuongeza uwajibikaji na hatimaye kuboresha utoaji huduma za kijamii katika maeneo yao”, alisema Bw. Nyela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) nchini, Bw. Peter Malika alisema shirika lao limeweka kipaumbele likishirikiana na serikali katika kusaidia kujenga uwezo na kuwekeza katika maendeleo ya ndani ili kufika malengo yaliyowekwa.
“Mwongozo huu utaweka viwango na kuziwezesha halmashauri na taasisi nyingine za serikali zinazoendesha biashara, kutumia muundo sahihi wa utawala bora ili kuboresha shughuli za miradi, utoaji huduma bora, kuongeza kwa ushiriki wa sekta binafsi na kukuza maendeleo ya ndani ya nchi”, alisema Bw. Malika.
Awali, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa TAMISEMI, Bw. John Cheyo alisema kupitia mwongozo huo wananchi watarajie mafanikio ya miradi ya kimkakati itakayowasaidia kupata huduma bora kama vile afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na nyinginezo.
Hafla ya uzinduzi huo ilitanguliwa na mafunzo ya siku mbili kuhusu matumisi ya mwongozo huu yalitolewa kwa maofisa 72 wa serikali kutoka mikoa tisa na halmashauri 16 yakiongozwa na wakufunzi kutoka UNCDF, TAMISEMI na Wizara ya Fedha. Huku yakihitajika kutolewa kwa halmashauri nyingine ii kuongeza uelewa na kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.