The House of Favourite Newspapers

Mzambia Ampa Ugumu Okwi Kutua Simba

0

UPO uwezekano mkubwa winga wa Al Ittihad Alexandria ya Misri, Mganda Emmanuel Okwi kutosajiliwa na Simba kwa msimu ujao ikiwa ni baada ya viongozi kugawanyika wakimtaka zaidi winga wa klabu ya Zanaco ya nchini Zambia, Moses Phiri kusajiliwa na timu hiyo.

 

Okwi na Phiri hivi karibuni walitajwa kuwaniwa na Simba katika usajili wa msimu ujao katika kutengeneza kikosi imara kitakachofanya vyema katika Ligi ya Mabingwa Afrika.Simba wanataka kumsajili winga mmoja hatari mwenye uwezo kama aliokuwa nao Luis Miquissone raia wa Msumbiji anayetajwa kuuzwa katika msimu ujao.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, ni ngumu Simba kumsajili Okwi ambaye hakuwa anapata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha Al Ittihad  Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, timu hiyo imepanga kufanya usajili wake kwa kigezo cha mchezaji anayepata nafasi ya kucheza katika klabu yake aliyokuwa anaichezea na siyo wa benchi.

Aliongeza kuwa upo uwezekano mkubwa wa Phiri kujiunga na Simba katika msimu ujao na tayari Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Hans Poppe anatajwa kutua Zambia kwa ajili ya kukamilisha dili hilo.

 

“Viongozi wamegawanyika hivi sasa wapo wanaomtaka Okwi na Phiri ambaye yeye ana nafasi kubwa ya kusajiliwa kutokana na kuwepo katika kiwango cha juu hivi sasa.

 

Okwi kinachompa ugumu wa kusajiliwa Simba ni yeye mwenyewe kupoteza nafasi ya kucheza katika timu yake anayoichezea huko Misri.

 

Hivyo bado viongozi wanaendelea kuvutana winga yupi asajiliwe kati ya hao wawili na lolote linaweza kutokea, nisubirie tuone baada ya dirisha la usajili kufunguliwa,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Zacharia Hans Poppe hivi karibuni alisema kuwa: “Nina idadi ya wachezaji 11 wa kigeni ambao wote wanaomba kuja kuichezea Simba, kati ya hao bado hatujaamua yupi tumsajili licha ya kuwepo katika mazungumzo na badhi ya wachezaji.”

Leave A Reply