Mzee Yusuf: Tukutane Dar Live Mkesha Wa Kuamkia Nanenane

ILE shoo babkubwa ya Narudi Mjini ya Mzee Yusuf kama Mzee Yusuf, iliyokuwa ifanyike Julai 31, mwaka huu, imesogezwa mbele kutokana na maombolezo ya kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa.

 

Shoo hiyo sasa itafanyika Julai 7, mwaka huu ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani wa Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar ambapo itakuwa ni siku ya mkesha wa kuamkia Sikukuu ya Nanenane.

 

Mzee Mkapa alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita hivyo kusimamisha shughuli za burudani kwa ajili ya maombolezo ambapo amepumzishwa kwenye nyumba yake ya milele kijijini Lupaso wilayani Masasi, Mtwara.

 

Akizungumza na IJUMAA SHOWBIZ, mratibu wa shoo hiyo, Rajab Mteta ‘KP’ amesema baada ya kusogezwa mbele kwa shoo hiyo, Mzee ametamka; “Sasa tukutane Dar Live Mkesha wa kuamkia Nanenane.”

 

KP amesema wameamua kusitisha shoo hiyo kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao ambapo wao kama uongozi wanaungana na Taifa kuomboleza kifo cha Mkapa, hivyo ni rasmi sasa kwamba shoo hiyo sasa itafanyika siku ya Mkesha wa Sikukuu ya Nanenane.

 

“Tumesogeza mbele kidogo, lakini hakuna kilichoharibika kwa sababu Mzee Yusuf ameahidi kufanya shoo ya kihistori na ametamka kwa mashabiki wake ‘tukutane Dar Live Nanenane’ hivyo siyo shoo ya kukosa.

 

“Tunawaomba mashabiki wote wa Mzee Yusuf wafike kwa wingi ndani ya Dar Live kwani siku hiyo Mfalme wa Taarab, mbali na sapraizi kibao pia atapata nafasi ya kutambulisha nyimbo zake mpya,” amesema KP.

 

Kwa upande wake Mzee Yusuf alikuwa na haya ya kusema; “Naomba mashabiki wangu wafike kwa wingi, kama mnavyojua huwa sina kazi mbovu mjini, mfalme narudi tena na narudi kwa kishindo kikubwa, nimejipanga kuwapa burudani ya kutosha.”

Toa comment