MZUKA WA SIMBA MAZEMBE WAMEPAGAWA!
TP Mazembe wamepagawa, zimwi la kutolewa na Simba linawaumiza kichwa kuelekea mchezo wa leo jioni. Ingawa wameonekana kulazimisha tabasamu, lakini mashabiki na viongozi wanahofi a kwamba Simba isije ikawalazimisha sare ya mabao na kuwaondoa kwenye hatua hii ya robo fainali kama msimu uliopita walivyotolewa. Msimu huo Mazembe walitolewa kwa suluhu ya ugenini na sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Ze Agosto ya Angola.
Pamoja na fi tna zote za nje ya uwanja, lakini Simba inashuka uwanjani leo jijini Lubumbashi kufanya maajabu yatakayoishangaza dunia na Kocha wa Simba, Patrick Aussems amewaambia mashabiki wavute pumzi. Matokeo ya suluhu kwenye robo fainali ya kwanza pale Dar es Salaam hayawatishi Simba.
Aussems na beki Zana Coulibaly wamewaambia wana Simba kwamba leo wanapindua meza kwa kupata sare ambayo itawapeleka nusu fainali kwani Mazembe wana presha sana. Langoni kama kawaida atasimama Aishi Manula, lakini ukuta wake utalindwa na Zana, Erasto Nyoni, Juuko Murshid na Asante Kwasi kwa sababau kuna hatihati ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kukosekana.
Hapo kati atakuwepo James Kotei, Jonas Mkude na Clatous Chama kama anaibiaibia. Mbele watakuwepo wazee wa kazi Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kegere. Kutokana na mbinu za mchezo huu, Haruna Niyonzima itabidi aanzie benchi asome ramani.
Itakavyokuwa leo hapa kwenye Uwanja wa Mazembe ni kwamba utajaa mashabiki waliokaa 18,500 tena waliovaa nguo nyeupe na nyeusi. Tabia yao ni kupiga makelele kwelikweli kuanzia sekunde
ya kwanza mpaka ya mwisho.
Kabla mpira kuanza, mashabiki wote husimama na kuongozwa na viongozi wao kuimba wimbo maalum wa klabu ambao wameutunga kuhamasishana. Wakati wanauimba wanashika kifuani na kunyoosha mkono mmoja tu. Baada ya hapo mgeni wa heshima anapita kuwasalimia mashabiki kwa kupiga makofi na wao wanajibu, uwanja mzima unasisimka wakiwa wamesimama hivyohivyo.
Kwenye mechi kubwa na muhimu kama ya leo huwa anafanya Moise Katumbi mwenyewe, lakini kwa vile bado yupo uhamishoni nchini Ubelgiji, mtoto wake atabeba majukumu. Simba wamesisitiza kwamba yote hayo wanayatambua na mchezo ni dakika 90, watapambana mpaka tone la mwisho na liwalo na liwe.
Kwenye mechi hiyo itakayochezwa saa 10 jioni, ni lazima kwa vyovyote vile hata kwa bao la mkono au sare mmoja afe na mwingine asonge nusu fainali.
MTIHANI
Simba inataka kuandika historia mpya kwenye mashindano hayo msimu huu, kwanza kwa kutinga nusu fainali lakini kushinda mechi ngumu ya ugenini kwa mara ya kwanza. Simba wanataka kutonesha kidonda cha Mazembe kutolewa na De Agosto ya Angola msimu uliopita kwenye hatua hiyo.
Mazembe walitoka suluhu ugenini, nyumbani wakalazimishwa sare ya bao 1-1, wakaaga mashindano hayo yenye utajiri mkubwa Afrika kwa ngazi ya klabu. “Kuna baadhi ya makosa yalijitokeza ambayo natakiwa kuyafanyia marekebisho ili kuwa na kikosi imara katika mchezo wa marudiano.
“Ninawajua wapinzani wangu, hivyo kwa sasa mawazo yangu yote ni katika mchezo wa ugenini japokuwa tunajua ugumu ambao tutakaokutana nao, natumia mchezo uliopita kukiandaa kikosi changu, kutakuwa na mabadiliko makubwa sana ya kiufundi, mambo hayatakuwa kama ilivyokuwa mechi zilizopita,” anasema Aussems.
Katika mechi tatu za ugenini za hatua ya makundi, Simba iliruhusu mabao matano kwa Ahly na mengine kama hayo mbele ya AS Vita, huku ikipigwa mabao mawili na JS Saoura. Mazembe hawajapoteza mchezo kwenye uwanja wao zaidi ya kutoka sare. Golini bado atakaa yuleyule Ibrahim Mounkoro raia wa Mali, na kule mbele Trésor Mputu, Rainford Kalaba na Jackson Muleka.
Ingawa mazoezi yao yalikuwa ya siri, lakini inaelezwa kwamba kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye
ulinzi ili kuepuka makosa ya Dar es Salaam.
SARE TU
Kwa namna yoyote ile hata kwa kufi a uwanjani, Simba inahitaji sare ya mabao ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo. Mazembe imekuwa ikijivunia mashabiki wake ambao imewajaza sumu kwamba timu yoyote ngeni inapoingia kwenye ardhi ya Lubumbashi waivuruge kisaikolojia kuanzia huko mitaani mpaka uwanjani siku ya mchezo wenyewe.
Mazembe waliamua kuwajaza sumu hiyo ya kufa na kupona mashabiki wao kutokana na mizengwe waliyokumbana nayo wakati wanapambana na timu kubwa za Uarabuni wakati Moise Katumbi anaanza uwekezaji kama wa Mohammed Dewji ‘Mo’. Zana Coulibaly anasema;
“Tunajua tutachofanya kwenye mchezo huu, kila timu bado ina nafasi ya kushinda kwa sababu kwenye mchezo wa kwanza hakuna aliyeweza kumfunga mwenzake.” Naye Aussems anasisitiza;
“Pia kikosi changu ambacho kitacheza na Mazembe natarajia kitakuwa na mabadiliko kwa kiasi kikubwa tofauti na kile ambacho kilicheza hapa na hii ni kutokana na hali ambayo ilijitokeza ya kupata majeruhi na adhabu za kadi na mengine yatakuwa ni ya kawaida tu.”


Comments are closed.