The House of Favourite Newspapers

Nabi Aanzisha Vita ya Makambo, Mayele Yanga SC

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi ni kama amechochea vita ya namba kwa washambuliaji wake Wakongomani, Fiston Mayele na Heritier Makambo kwa kutamka kuwa wachezaji wake hao wote wana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo icheze mchezo wake wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Zanaco FC ya Zambia uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar huku Mayele akianzia benchi aliyeingia badala ya Makambo.

 

Washambuliaji hao hadi hivi sasa kila mmoja amefunga bao moja katika michezo ya kirafiki waliyocheza, juzi Mayele alifunga bao moja walipocheza dhidi ya Friends Rangers inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza huko Uwanja wa Avic Town, Kigamboni.

 

Mmoja wa mabosi wa Yanga kutoka kwenye Benchi la Ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, kocha huyo alifanya kikao cha wachezaji na kuwaongezea morali ya kila mchezaji kupambana ili apate nafasi ya kucheza katika kikosi ikiwemo hiyo ya ushambuliaji inayochezwa na Mayele, Makambo, Ditram Nchimbi na Yusuph Athumani.

 

Aliongeza kuwa ili mchezaji apate nafasi ya kucheza, ni lazima amuonyeshee katika mazoezi yake kwa kuhakikisha anatimiza majukumu yote ya ndani ya uwanja atakayompa.

 

“Ngumu kwa Fei Toto (Salum Abdallah) kuanzia benchi kwa hivi sasa, hiyo ni kutokana na ubora aliokuwa nao na majukumu makubwa aliyopewa na kocha Nabi ambaye amemuamini na kumhamisha kutoka namba sita na kumchezesha kumi.

 

“Hivyo Makambo na Mayele mmojawapo ni lazima ataanzia nje katika kikosi chake cha kwanza ambao wote wanacheza namba tisa, labda itokee abadili mfumo wa kutaka kuwatumia washambuliaji wawili katika mechi.

 

“Hivyo kocha amewapa nafasi wachezaji wote ya kupambania kucheza katika kikosi chake kwa kuwaambia hakuna mshambuliaji mmoja maalum wa kumtegemea zaidi ya yule atakayepambana ndiye atakayekuwa anamuanzisha,” alisema bosi huyo.

 

Akizungumzia kambi ya timu hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli, ameliambia gazeti hili: “Kambi ya mazoezi inaendelea vizuri huko Avic, kocha anaendelea kutengeneza muunganiko wa timu baada ya kuona upungufu mchezo uliopita wa kirafiki dhidi ya Zanaco.

 

“Kocha anafurahia ushindani wa namba kutoka kwa vijana wake akiamini ndani ya muda mfupi timu itakaa sawa baada ya usajili mkubwa uliofanywa wa wachezaji wapya.”

 

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

 

Leave A Reply