Kartra

Nabi Aiweka Kiporo Simba

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amefunguka kuwa kwa sasa haufikirii kabisa mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba utakaopigwa Septemba 25, mwaka huu badala yake mawazo yao yote wameyaelekeza kwenye michezo yao miwili ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

 

Yanga wamepangwa kucheza dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo mchezo wa kwanza unatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Septemba 12, na kurudiana Septemba 19, Nigeria.

 

Baada ya kumalizana na Wanaigeria hao, Yanga watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii, ambao kikanuni huwa ndio ufunguzi rasmi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Nabi alisema: “Najua tuna mchezo mgumu dhidi ya Simba ndani ya mwezi huu wa Septemba katika Ngao ya Jamii, lakini hatuufikirii kabisa mchezo huo kwa kuwa tuna kazi kubwa ya kuifanya katika michezo yetu ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

“Tumeweka mawazo yetu yote katika kuhakikisha tunashinda michezo hiyo miwili ili kufuzu kwenda hatua inayofuata ya michuano hiyo, baada ya kumaliza majukumu hayo hapo ndipo naweza kuzungumza kuhusiana na mchezo wetu dhidi ya Simba.”

JOEL THOMAS, Dar es Salaam


Toa comment