The House of Favourite Newspapers

Nabi Aja na Mbinu Mpya za Ushindi

0

BAADA ya kuchezea kipigo cha kwanza katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi ataingia uwanjani kivingine kuwavaa Tanzania Prisons.

 

Yanga, leo Ijumaa inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa katika mchezo wa Hatua ya 16 wa Kombe la FA.

 

Huo ni mchezo wa pili kwa Nabi kukaa kwenye benchi la ufundi tangu ajiunge na timu hiyo wiki moja iliyopita kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, kocha wa makipa wa timu hiyo, Razack Siwa alisema Nabi ameanza mikakati mipya na safu yake ya ushambuliaji baada ya kuona wanakosa umakini katika mchezo uliopita dhidi ya Azam FC.

Siwa alisema kuwa timu yao inatengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini umakini mdogo wa washambuliaji wake ndiyo unasababisha wao washindwe kupata matokeo mazuri ya ushindi.

 

Siwa alisema Nabi amewaambia wachezaji wake anataka soka la kushambulia na washambuliaji kuongeza umakini na utulivu wanapopata nafasi za kufunga wanapofika ndani na nje ya 18.

 

“Hivi sasa kila mchezaji amepewa majukumu yake ya kuhakikisha tunaenda kufanya vizuri kwenye mchezo wa kesho (leo) wa FA dhidi ya Prisons hasa katika umakini wa safu ya ushambuliaji kuhakikisha wanatumia nafasi wanazozipata.

 

Kwani timu inapopoteza nafasi ya wazi ngumu kuipata nyingine hivyo ni lazima umakini uongezeke kwa washambuliaji wetu wanapokuwa uwanjani.“Kocha Nabi hataki kuona timu inapoteza mchezo wa pili mfululizo wakati tukielekea kucheza dhidi ya Prisons ambao tunaamini nao wamejiandaa kupata matokeo mazuri,” alisema Siwa

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply