The House of Favourite Newspapers

Nabi Atoa Agizo Zito kwa Diarra, Aucho

0

WAKATI Klabu ya Yanga jana ikicheza mechi nyingine ya ndani ya mazoezi dhidi ya Pan African SC jana, kujiwinda na mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Nasreddine Nabi, amewataka mastaa wake waliopo timu ya taifa nje ya nchi kukwea pipa mara moja pindi tu mechi yao kesho itakapomalizika.

 

Mbali na mechi moja ya kirafiki ya kimataifa iliyocheza Siku ya Kilele cha Mwananchi dhidi ya Zanaco FC ya Zambia na kupoteza kwa mabao 2-1, wiki iliyopita Yanga ilicheza mechi nyingine ya ndani ya kirafiki ya mazoezi dhidi ya Friends Ranger FC ya Manzese, Dar es Salaam na kushinda kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Avic Town ilipo kambi yao.

 

Na jana jioni ilicheza mechi nyingine ya kirafiki ya mazoezi dhidi ya Pan African kwenye uwanja huo, lengo likiwa ni lile lile la kujiandaa mechi yao ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria itakayopigwa Jumapili wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

 

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema tayari Kocha Nabi, amewataka wachezaji wake wawili waliopo nje ya nchi kuzitumikia timu zao za taifa, kiungo Khalid Aucho wa Uganda na kipa Djigui Diarra kukwea pia mara moja pindi tu mechi yao itakapomalizika leo.

 

Uganda leo itaikaribisha Mali kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia nchini Qatar mwakani, na timu hizo zitakutana nchini Uganda baada ya mechi za awali Waganda kulazimisha sare tasa ugenini dhidi ya Kenya na Mali kuichapa Rwanda.

 

“Kwa ujumla maandalizi kuelekea mechi yetu ya kimataifa Jumapili, yanaendelea vizuri na wachezaji wote wapo fiti, hatuna majeruhi yeyote. Leo (jana) jioni tutacheza mechi nyingine ya mazoezi ya kirafiki dhidi ya Pan African ya Dar es Salaam.

 

“Kikubwa kocha alichoagiza ni kwa wachezaji wake wawili Aucho na Diarra, kuhakikisha wanaanza safari mara moja baada ya mechi yao ya kesho (leo) kumalizika ili kuwahi kuendelea na maandalizi na wenzao,” alisema Bumbuli.

 

Kuhusu uwezekano wa kupata mechi nyingine ya ndani ama ya kimataifa ya kirafiki kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Rivers United, Bumbuli alisema itategemea na maamuzi ya kocha lakini kwa sasa hajaagiza.

 

“Kwa upande wa mechi ya kimataifa ya kirafiki, hilo halipo kabisa kwa sababu siku ni chache haiwezekana kuanza kulishughulikia hasa ukizingatia wachezaji mpaka waanze kupimwa COVID-19 ili kupata kibali, hilo litakuwa ni vigumu, kama umelisikia hizo ni habari za mitaani tu hazina ukweli wowote.

 

“Lakini kama kocha atakuwa na mahitaji ya kupata mechi nyingine ya kirafiki ya ndani atatafutiwa ila bado hajasema,” alisema Bumbuli.

 

Mbali na nyota hao wawili walipo nje ya nchi, wachezaji wengine wa Yanga ambao wanakosekana kambini ni Kibwana Shomari, Bakari Mwamunyeto, Dickson Job na Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambao wapo nchini na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa kuikaribisha Madagascar katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Leave A Reply