The House of Favourite Newspapers

Nabi Awaandalia Programu ya Mabao Mayele, Makambo

0

KOCHA mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amekiri kuwa ni kweli safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na washambuliaji Fiston Mayele na Heritier Makambo, imekuwa na tatizo la kukosa umakini na kupoteza nafasi nyingi za wazi na kuahidi kuwaandalia programu maalum ya kuhakikisha wanafunga mabao mengi zaidi.

 

Yanga Jumamosi walifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ushindi ambao umewafanya kufikisha pointi sita na kuwaweka kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kabla ya michezo juzi.

 

Licha ya ushindi huo, Yanga wameonekana kuwa na shida katika safu yao ya ushambuliaji ambapo katika michezo hiyo mitatu dhidi ya Simba, Kagera Sugar na Geita Gold wamefunga mabao matatu tu, bao moja kwenye kila mchezo.

 

Akizungumza  na Championi Jumatatu, Nabi alisema: “Tulikuwa na mchezo mzuri dhidi ya Geita Gold na kufanikiwa kupata pointi tatu muhimu, kwangu nawapongeza sana wapinzani wetu kwa ushindani waliotuonyesha.

 

“Licha ya ushindi huo lakini ni wazi bado tuna changamoto katika safu yetu ya ushambuliaji hasa kutokana na nafasi nyingi za mabao tulizokosa, lakini tumechukua changamoto hiyo na tutalifanyia kazi naamini katika michezo ijayo tutafunga mabao mengi zaidi.

 

“Kuhusu kwa nini Makambo anaanzia benchi naweza kusema tuna washambuliaji watatu wazuri na kwa sasa tunaanza na Fiston Mayele lakini naamini muda utafika Makambo na Yusuph Athumani watapata nafasi.”

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave A Reply