The House of Favourite Newspapers

Nabi Azigomea Kambi Arusha, Zanzibar

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasraddine Nabi, ameugomea uongozi wa timu hiyo, kuhusiana na suala la kutaka kuiweka timu hiyo kambi nje ya Jiji la Dar es Salaam, kama walivyopendekeza wajumbe wa kamati ya mashindano kwenda Arusha, Zanzibar au kubaki Dar.

 

Yanga ipo mapumziko kwa takribani wiki mbili kufuatia Ligi Kuu Bara kusimama kupisha mechi za timu ya taifa ambapo baadhi ya nyota wake wamejumuishwa kwenye vikosi mbalimbali vya mataifa yao.

 

Chanzo chetu kutoka ndani ya kambi ya timu hiyo iliyopo Avic Town, Kigamboni mkoani Dar, kimebainisha kuwa, Kocha Nabi ameigomea kamati ya mashindano baada ya kumtaka kocha huyo achague kati ya sehemu tatu ambazo angependa kuweka kambi na kikosi hicho.

 

Taarifa ya awali ya Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli iliweka wazi kuwa, kikosi hicho kilitakiwa kusafiri kwenda jijini Arusha kwa ajili ya kambi ya wiki mbili na sasa jambo hilo halitakuwepo tena.

 

“Kamati ya mashindano iliona ni vyema kutoa nafasi kwa kocha ya kumtaka achague kati ya Zanzibar, Arusha au kubaki Dar kwa ajili ya maandalizi ya wiki mbili, ambapo kocha amewaambia hataenda kokote na badala yake kambi ataifanyia Dar.

 

“Kabla ya ligi kusimama kamati ya mashindano iliona ni vyema kumpatia fursa ya utulivu kocha kwa kumruhusu achague mahali pa kukinolea kikosi chetu lakini amegoma kutoka Dar es Salaam, kwa kuogopa kuwachanganya wachezaji kwa muda mfupi wa wiki mbili,” kilisema chanzo hicho.

 

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Rodgers Gumbo alisema: “Kweli timu haitaenda tena Arusha kutokana na baadhi ya wachezaji wetu wa kimataifa paspoti zao kuisha muda hivyo wamerejea kwao ili kwenda kutengeneza mpya,”.

Joel Thomas, Dar es Salaam

Leave A Reply